Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema Serikali ya Tanzania, China na Uholanzi zitaendelea kushirikiana kukiendeleza Kituo cha Taasisi ya Utafiti na Uendelezaji wa Mazao ya Mbogamboga Duniani cha World Vegetable Centre ili kukidhi mahitaji ya wakulima.

Mweli amesema hayo wakati akizundua Benki ya Afrika ya vinasaba ya mbegu za mboga za asili katika kituo cha Worldveg kilichopo Tengeru mkoani Arusha na kuwataka watafiti kutumiza majukumu yao kikamilifu ili benki hiyo isiwe ya makumbusho kwani uhifadhi ya mbegu unapaswa kuwasaidia wakulima Afrika.

Amesema hadi sasa benki hiyo inahifadhi aina 5,000 ya mbegu lakini hadi kufikia 2025/26 aina 15,000 ya mbegu zinapaswa kuhifadhiwa katika benki hiyo na kazi kubwa inapaswa kufanywa na watafiti ili mbegu hizo za asili za mboga ziweze kuwafikia wakulima wengi Afrika na dunia.

Katibu Mkuu amesema msingi wa kituo hicho ni kwa ajili ya wakulima duniani na sio Afrika pekee yake hivyo basi jitihada za ziada zinahitajika kwa wataalamu wa utafiti kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili mbegu za asili za mboga ziweze kuwasaidia wakulima mashambani.

Amesema mbegu za asili za mbogamboga zinapaswa kutuzwa katika benki hiyo ya pili duniani ili kizazi kijacho kiweze kujua historia ya mbegu hiyo na watafiti wanapaswa kufanya utafiti wa sasa na utafiti wa kizazi kijacho kwa maslahi ya wakulima.

‘’Tuhifadhi mbegu kwa ajili ya tafiti bora kwa ajili ya wakulima na tusihifadhi mbegu kwa ajili ya maonyesho ya makumbusho hilo haliwezekani’’amesema Mweli.

Katibu Mkuu Mweli amesema Serikali itatoa eneo lingine kwa ajili ya Worldveg kwani eneo walilonalo la ekari 14 haitoshi kwani limejaa kwa ajili ya matumizi ya tafiti na bustani za mafunzo za mbogamboga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Worldveg Afrika, Gabriel Rugalema aliwashukuru wafadhili wote waliofanikisha ujenzi na uletaji wa vifaa vya kisasa katika Benki ya Vinasaba vya mbegu na kusema kuwa taasisi hiyo haiwatawaangusha kwani watafanya kazi kwa kujituma kwa ajili ya wakulima na kuinua uchumi wa wakulima Afrika.

Rugalema alisema Benki ya Vinasaba vya mbegu Afrika ni benki pekee Afrika hivyo ni sifa kwa Tanzania na Afrika na watatumia nafasi hiyo kutunza,kukuza na kuendeleza mbegu za asili za mboga mboga kwa maslahi ya wakulima.

Alisema na kuwataka wanasayansi kutumia nafasi ya uwepo wa Benki ya Vinasaba ya mbegu Afrika katika tafiti mbalimbali lengo likiwa moja la kutaka wakulima kuwa na mbegu bora yenye kuwanufaisha katikamazingira tofauti ya ukame na mabadiliko ya tabia nchi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Worldveg Duniani, Marco Wopereis amewashukuru wafadhili wote wanaoshirikiana na kituo hicho katika kufanya utafiti wa kisasa wa mbegu na kuwataka kuendelea na moyo huo wa kuendelea kukuza na kuendeleza kilimo cha mboga mboga duniani.