#Dkt. Biteko awasilisha salamu za Rais Samia miaka 61 ya Uhuru wa Uganda

Na Neema Mbuja, JamhuriMedia, Kampala

Serikali ya Tanzania imeahidi kuendeleza Ushirikiano, Umoja na Mshikamano na nchi ya Uganda kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Nchi ya Uganda yaliyofanyika Oktoba 9, 2023 kwenye Viwanja vya Kitgum kaskazini mwa nchi ya Uganda.

Akitoa salamu hizo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Biteko amesema kuwa Rais anathamini mchango na maendeleo yaliyofikiwa na nchi ya Uganda katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi.

“Mhe Rais anakupongeza Sana kwa siku hii muhimu ya miaka 61 ya Uhuru na wananchi wote wa Uganda na ameahidi kuendelea kishirikiana katika kujenga uchumi wa nchi hizi mbili na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Aidha, Rais amemshukuru Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa jitihada zake za kudumisha umoja na mshikamano kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania na Uganda zimekuwa na mahusiano na ushirikiano wa muda mrefu kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga, pamoja na miradi mbalimbali kwenye sekta ya Nishati, Utalii, Kilimo,

Historia ya nchi hizi mbili ilianza tangu kipindi cha harakati za Uhuru baina ya waasisi wa nchi hizi mbili na ushirikiano huu unaendelezwa na kudumishwa kwa umoja, amani, mshikamano na utu uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Hafla ya miaka 61 ya Uhuru wa Uganda ilihudhuriwa na Makamu wa Rais Burundi Prosper Bazombanza, Wawakilishi kutoka Jumuiya ya falme za kiarabu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Kenya Peter Mathuki, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Uganda, Mawaziri, wabunge kutoka nchini Uganda na wananchi wa nchi hiyo.

By Jamhuri