Tanzania yawakaribisha wawekezaji kutoka Urusi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Serikali ya Urusi kuwekeza nchini kwa maslahi ya pande zote mbili na ustawi wa dunia kwa ujumla.

Mwaliko huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) wakati aliposhiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Urusi jana jioni Jijini Dar es Salaam.

“Tanzania ina mazingira tulivu ya biashara na uwekezaji yanayotoa fursa za uwekezaji, hivyo natoa rai wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Urusi kuja kuwekeza Tanzania ili kuimarisha zaidi biashara baina ya nchi zetu mbili,” alisema Balozi Mbarouk.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Urusi jana jioni (tarehe 14 Juni, 2023) Jijini Dar es Salaam. kushoto ni Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Tanzania kwa kushirikiana na sekta binafsi zimeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha kuwa uwekezaji unafanyika katika mazingira rafiki na salama na kuwafanya wafanyabiashara kutoka nje kufanya biashara zao katika mazingira salama na rafiki.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Urusi imekuwa mshirika wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na kisiasa nchini Tanzania. Kwa kusainiwa kwa mkataba wa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Kiserikali ya Biashara na Ushirikiano wa Kiuchumi, nchi hizo mbili zipo katika nafasi nzuri zaidi ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi wa Urusi nchini, Andrey Avetisyan alisema kuwa ushirikiano wa Urusi na Tanzania ni wa kihistoria na umekuwa imara wakati wote. Urusi itaeendelea kushirikiana na Tanzania kijamii, kisiasa na kiuchumi wakati wote.

“Tunapoadhimisha siku hii muhimu tunakumbuka pia miaka 62 ya uhusiano kati ya Urusi na Tanzania. Aidha, Balozi Avetisyan aliongeza kuwa Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Avetisyan.

“Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha biashara na uwekezaji ambapo kwa sasa ukuaji wa biashara baina ya mataifa yetu umeongezeka. Tunaendelea kuboresha biashara licha ya changamoto zinazojitokeza,” aliongeza Balozi Avetisyan.

Tanzania na Urusi zinashirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi, afya, biashara, viwanda, uwekezaji na utalii ambapo kwa pamoja zimekubaliana kuendeleza ushirikiano huo ili kuleta tija katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiaana na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Avetisyan wakati maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Urusi jana jioni (tarehe 14 Juni, 2023) Jijini Dar es Salaam
 
Balozi wa Urusi nchini, Andrey Avetisyan akizungumza na washiriki wakati maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Urusi jana jioni (tarehe 14 Juni, 2023) Jijini Dar es Salaam