Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA), imetoa misaada mbalimbali ikiwemo unga tani 6.4, maharage kilo 666, magodoro 186 vyenye thamani ya 20mil kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji.

Aidha imetoa imetoa boti moja kwa ajili ya kuongeza msaada kwa vyombo vya uokoaji.

Akimkabidhi msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakar Kunenge, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi (TAWA), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Kusini Mashariki SACC ,Abraham Jullu, alitoa pole kwa wananchi wa Rufiji na Kibiti .

Ameeleza, licha ya msaada wa chakula na magodoro mamlaka hiyo imetoa boti ili kuongeza msaada kwa vyombo vya uokoaji na kusema kwamba wameendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya tahadhari ya wanyama ( mamba na viboko).

Amefafanua ,hadi kufikia aprili 15,2024 wametoa elimu kwa wananchi 4,226 katika kata nne wilayani Rufiji.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kunenge ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka hiyo chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi (TAWA) Mej. Gen. Hamisi Semfuko na Kamishna wa Uhifadhi (TAWA) Mabula Misungwi kwa namna ambavyo (TAWA) ilivyojitoa kushirikiana na wananchi wa Rufiji na Serikali katika athari za mafuriko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle aliishukuru TAWA kwa kuwa karibu na wananchi wa Rufiji hata kabla ya athari za mafuriko huku akimtaja Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa kuwa ndiyo kinara wa ushirikiano huo kati ya Taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo.

By Jamhuri