DAR ES SALAAM
NA MICHAEL SARUNGI
Ujio wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino,
hapa nchini unaweza kuwa na matokeo mazuri katika soka la nchi hii endapo
viongozi watakuwa na utashi wa kutenda.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti juu ya ziara hiyo, wadau wa
mchezo huo wamesema ziara hiyo ya kiongozi huyo mkuu wa FIFA, inaweza
kuwa ni historia endapo patakosekana mipango ya dhati.
Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba, Hassan Dalali, amesema Tanzania
inaweza kuwa katika ramani ya mchezo wa mpira kama viongozi wa soka
watakuwa na mipango endelevu ya kukuza vipaji.
Amesema ziara hiyo ya kiongozi huyo inaweza ikawa ni fursa nzuri kuanzia kwa
klabu, wachezaji na TFF kutokana na kuwa dunia nzima ya wapenda soka
watakuwa wanaijua Tanzania.
Amesema ujio huo umeleta fursa nzuri na kufungua milango kwa viongozi wa
mchezo huo na wachezaji, kuweza kufahamika katika ulimwengu wa wapenzi wa
mchezo huo hapa nchini na duniani kote kwa ujumla.
Amesema pamoja na ajenda kuu katika mkutano huo kuwa ni ufadhili katika eneo
la maendeleo ya mpira, lakini ni fursa kubwa pia na muhimu kwa maendeleo ya
mpira wa nchi hii.
Amesema katika nchi nyingi za Kiafrika kuna matatizo makubwa katika suala zima
la ukuzaji wa vipaji vya vijana wadogo kutokana na ukosefu wa fedha, hivyo
kitendo cha Rais wa FIFA kuahidi ufadhili ni ishara nzuri.
Amesema kitendo cha Tanzania kushindwa kupata mafanikio katika mpira tangu
mwaka 1980 iliposhiriki kwa mara ya kwanza na mwisho fainali za Afrika mjini
Lagos, Nigeria huenda ikafikia mwisho.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga, amesema ujio
wa Rais wa FIFA, Infantino, ni ishara nzuri kwa soka la Tanzania.
Amesema mchezo wowote ule unahitaji uwekezaji wa fedha kama nchi inahitaji
kupata maendeleo, hali ambayo imekuwa kikwazo cha maendeleo ya mchezo huo
katika nchi nyingi za barani Afrika.
Amesema mojawapo ya faida ya ujio wa viongozi wa FIFA nchini ni nyingi, lakini
kikubwa zaidi ni ujenzi wa viwanja katika mikoa tisa ya Tanzania na lengo ni
kuona mpira unachezwa kila mahali.
Amesema mpira hauwezi kuendelea kwa kuchezwa katika miji ya Mkoa wa Dar es
Salaam pekee, Mwanza na miji mingine unapaswa kusambaa hadi vijijini ili kupata

vipaji zaidi.
Kocha wa Njombe Mji, Ally Bushiri amesema ujio wa FIFA nchini ni neema
ambayo ikitumiwa vyema inaweza kuwazalisha akina Peter Tino, wengine wapya
watakaoweza kuja kuweka historia nyingine katika soka.
Amesema ahadi iliyotolewa na Rais wa FIFA ya kujenga viwanja vya soka katika
mikoa tisa nchini, inaweza kuirudisha Tanzania katika ramani ya soka la ushindani
kama ilivyokuwa zamani.
Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, amesema kinachotakiwa ni TFF
kuhakikisha mpira unaanza kuchezwa hata katika maeneo yaliyosahaulika hasa
katika maeneo ya vijijini, ili kuvumbua vipaji zaidi kwa ajili ya klabu na timu za
Taifa.
Amesema njia pekee na nyepesi kuweza kufikia malengo tarajiwa ya kupata
maendeleo katika mchezo wowote ule, ni kuhimiza katika uwekezaji kwa vijana
ambao baadaye watakuwa tegemeo katika klabu na timu za taifa.
Mwisho
Ends

Please follow and like us:
Pin Share