KAMISHINA wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. DoS Santos Silayo amewata wakulima kulima na kutunza mazingira ili kuendelea kupata mvua za kutosha.

Ni katika Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji, Prof Silayo amesema kuwa Watanzania wanatakiwa kuendelea kuvitunza vyanzo vya maji na mazingira kwa faida ya Taifa na dunia kwa ujumla.

Prof.Silayo amesema wakulima na wafugaji wamekuwa wakiharibu mazingira na vyanzo vya maji kwa kilimo na ufugaji ambao hauna tija kwa wananchi wengi kwa kuwa wamekuwa wakiharibu mazingira bila sababu ya msingi.

Amewataka wananchi kupinga vikali kwa wananchi wengine ambayo wamekuwa wakiharibu mazingira kwa makusudi na kusababisha majanga kwa binadamu na wanyama.

Amesema mahitaji makubwa ya nishati ikiwamo kuni na mkaa imekuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa misitu.

Amesisitiza kuwepo kwa nishati mbadala itakayosadia uhifadhi wa mazingira hasa mazao ya miti.

Profesa Silayo amefafanua kuwa tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 73 ya uharibifu wa misitu zinatokana na shughuli za kilimo.

Alikumbushia mwaka 1976 wakati wa Azimio la Iringa lililokuwa linaitwa Siasa ni Kilimo, umuhimu wa uhifadhi wa misitu ulitajwa kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa maji.

Hata hivyo alisisitiza kuwa wakati wa Uhuru, Tanzania ilikuwa na misitu 11 iliyohifadhiwa lakini sasa imeongezeka hadi kufikia 24, ukiwemo Msitu wa Hifadhi wa Saohill.

Profesa Silayo alisema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii na mikakati mbalimbali ya kusaidia kuwepo kwa uhifadhi wa mazingira.

“Wapo watu wanaamini kwamba kuchoma moto hovyo ni kuwasiliana na Mungu, lakini mwaka huu wamechoma na mvua haijanyesha, mvua ikinyesha Imani hiyo huwa inaendelea,” amesema Profesa Silayo.