Mamlaka ya Hali ya Hali ya Hewa nchini TMA, imetangaza kuwa msimu wa mvua za masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani huku maeneo mengine yakipata mvua za wastani hadi juu ya wastani

Akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi za TMA-Dar es Salaam,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt.Ladislaus Chang’a amesema maeneo yatakayopata mvua za juu ya wastani ni pamoja na Dar es salaam mkoa wa Pwani,Unguja na Morogoro kaskazini.

Aidha, ameongezea kuwa Ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Mei 2023, hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini

Mvua za masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi machi 2023 na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei 2023” amesema Dkt Chang’a.

Dkt. Changa amezitaja athari zinazotarajiwa kuwa ni mvua chache na zenye mtawanyiko usioridhisha katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani zinaweza kusababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo na upatikanaji wa maji kwaajili ya shughuli za kilimo

DKT Chang’a amesema mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa hivyo viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi hivyo ni vyema kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari zinazotolewa na TMA.

Awali Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Rose Senyangwa amesema mifumo ya hali ya hewa joto la bahari la wastani hadi juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la kati la bahari ya pasifiki, joto la wastani linatarajiwa katika eneo kubwa la kitropiki la bahari ya Hindi huku joto la juu ya wastani likitarajiwa katika eneo la Mashariki mwa Bahari ya Atlantiki hali hiyo itadhoofisha mifumo inayosababisha mvua.

Hata hivyo kwa mwaka 2022 utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ulifanikiwa kwa kiwango cha asilimia 94 hivyo wataendelea kutoa mrejesho wa mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika na kuwashauri wadau kuwasiliana nao ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaja maalum katika sekta zao.

By Jamhuri