Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA),imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ambapo imejipangia kutekeleza mikakati kadhaa itakayisaidia utoaji huduma za hali ya hewa nchini

Hayo yamebainishwa leo Novemba 2, 2022 jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzu wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt.Hamza Kabelwa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzu wa Huduma ya Hali ya Hewa Dkt.Hamza KabelwaMamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali GN.459 la Juni 14, 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu, kudhibiti na kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mamlaka hii imetokana na iliokuwa Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania ilioanzishwa kwa Sheria ya Wakala (Executive Agencies Act) Sura Na. 245 marejeo ya mwaka 2002. Kabla ya Wakala wa Hali ya Hewa, huduma za hali ya hewa nchini zilikuwa zinatolewa na iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa nchini (Directorate of Meteorology) ambayo ilianzishwa Mwaka 1978 baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ikiwa na jukumu la kufanya uangazi na kutoa taarifa za hali ya hewa nchini. Kabla ya Jumuiya ya Afrika Mashariki huduma za hali ya hewa nchini zilitolewa chini ya Taasisi ya Hali ya Hewa iliyokuwa chini ya wakoloni.

Kabelwa amesema kuwa majukumu ya Mamlaka yamegawanyika katika sehemu kuu tatu; sehemu ya kwanza ni kutoa huduma za hali ya hewa; sehemu ya pili ni kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha kumi na nne (14).

Sehemu ya tatu ni kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini Tanzania kulingana na Kifungu cha tano (5) cha Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019.

Aidha, Mamlaka ina jukumu la kuiwakilisha nchi katika masuala ya kiufundi (technical matters) ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.

Pamoja na utelezaji huo kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya Mwaka 2019, vilevile, Mamlaka imekuwa ikifuata miongozi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SGDs), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano iii 2021/22-2025/26, Ilani ya Chama cha Mapinduzi 200-2025 na Mpango Mkakati wa TMA.

Amesema kuwa katika katika utelekezaji wa majukumu yake katika mwaka wa fedha 2021/22 Mamlaka ya Hali ya Hewa imepata mafanikio mengi kama mamlaka iliendelea na utekelezaji wa mradi wa Rada, Vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ambapo hatua mbalimbali zilifikiwa.

“Hatua hizi ni pamoja na kukamilika kwa asilimia 90 ya utengenezaji wa mtambo wa rada mbili (2) za Mbeya na Kigoma ambapo pia malipo ya asilimia 90 yalifanyika.

“Mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia Rada hizo yalifanyika kiwandani nchini Marekani; ujenzi wa miundombinu ya Rada za Mbeya na Kigoma umekamilika; utengenezaji wa Rada mbili (2) za mwisho zitakazofungwa KIA na Dodoma ulifikia asilimia 45 ambapo Mamlaka ilifungua barua ya dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya utengenezaji wa Rada hizo,” amesema mkurugenzi huyo.

Amesema kuwa kukamilika kwa Rada hizi kutakamilisha mtandao wa Rada nchini kwa idadi ya Rada saba. Rada hizi zinauwezo wa kuona zaidi ya kilometa za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250. Aidha, mitambo hii pia inasaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisi wa anga letu la Tanzania.

Ameongeza kuwa utekelezaji mwingine ni kufungwa kwa mitambo miwili ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika na “measuring cylinders” zipatazo 100; Seti tano (5) za vifaa vya kutambua matukio ya radi; Vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa; vifaa 25 vya kupima kiasi cha joto na unyevunyevu; mitambo minne (4) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe; vifaa vya kupima mvua vinavyojiendesha vyenyewe.

“Aidha, Mamlaka imepokea kompyuta maalum “Cluster Computer” ambayo ipo katika hatua ya ufungaji; Vilevile Mamlaka ilizinduwa mfumo mpya wa uangazi wa hali ya hewa ya anga ya juu katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga ya juu kilichopo JNIA.

“Mamlaka iliingia mkataba wa ununuzi wa vifaa na mitambo mbalimbali ya hali ya hewa ikiwemo mitambo nane (8) ya kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga; mitambo 13 ya kupima hali ya hewa mahususi kwa sekta ya kilimo. Aidha, Mamlaka ilifungua hati ya dhamana (Letter of Credit) ya asilimia 80 kwa ajili ya mitambo hiyo,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa mamlaka imeendelea kutekeleza jukumu la kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku 5, siku 10, msimu na tahadhari ambapo usahihi wa utabiri katika kipindi husika ulikuwa asilimia 93.8 ukiwa juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika kimataifa;

Pia huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga ziliendelea kutolewa kwa kuzingatia mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (ISO 9000:2015) ambapo jumla ya ndege 40,323 zilihudumiwa katika mwaka 2021/22 ukilinganisha na ndege 35,111 zilizohudumiwa katika mwaka 2020/21 ambalo ni ongezeko la asilimia 13.

“Ongezeko hili linatokana jitihada za kuifungua nchi zinazofanywa na serikali yetu pamoja kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa na kuhakikishia dunia usalama wa anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kwa ndege zote za kimataifa;

“Mamlaka imeendelea na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kupitia ofisi zake zilizopo kwenye Bandari za Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika. Huduma hizi zimechangia kuongezeka kwa usalama na ufanisi wa shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye maji ikiwemo usafiri, shughuli za bandari, uvunaji wa gesi asilia n.k. Katika mwaka 2021/22, idadi ya watumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya maji iliongezeka na kufikia 36,774 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na watumiaji 32,736 waliohudumiwa katika mwaka 2020/21.

Kabelwa amesema kuwa kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa kumetokana na utekelezaji wa Sheria Na. 2 ya mwaka 2019 ambapo lengo ni kuboresha huduma na pia utoaji wa elimu kwa umma juu ya kutumia taarifa za hali ya hewa.

Amongeza TMA imeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake iliyopewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya kuwa Kituo cha kutoa mwongozo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa Ziwa Victoria (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Pia jukumu lingine la kimataifa ni kusaidia ufuatiliaji wa ubora na upatikanaji wa data za hali ya hewa kwa vituo vya hali ya hewa vilivyo katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Sudan ya Kusini kupitia kituo cha Kanda kilichopo Tanzania. Matukio mbalimbali ya kutopatikana kwa data yaliripotiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa ajili ya kupata msaada zaidi na pia kiliendelea kutoa ripoti za kila mwezi ambazo zilitumwa kwa nchi za Afrika Mashariki.

Amesema kuwa katika utekelezaji wa mwaka wa fedha wa 2022/23, Mamlaka ya Hali ya Hewa imepanga mikakati kadhaa itakayosaidia katika utoaji wa huduma za Hali ya Hewa Nchini. Baadhi ya Mikakati hiyo ni kama Kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa huduma za hali ya hewa.

Pia kuendelea na utekelezaji wa Sheria Na.2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake;Kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika Bahari na Maziwa Makuu ili kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia;

Kufanya ufuatiliaji kwa wakandarasi wanaotengeneza Rada na vifaa vya hali ya hewa ili vikamilike na kuwasili nchini;Kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa;uhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake.

Kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa
na Kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

By Jamhuri