Katika makala ya leo tutaona jinsi Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) jinsi inavyoweka mazingira wezeshi kibiashara na kuboresha maisha ya Watanzania kuelekea uchumi wa viwanda. 

Katika kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanawezeshwa kupitia bandari, serikali iliamua kuwekeza katika bandari za Ziwa Nyasa kwa kutekeleza miradi mbalimbali. Miradi hiyo ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa mitatu; ujenzi wa meli tatu na miradi miwili ya upanuzi wa Bandari ya Kiwira. 

Serikali kupitia TPA iliamua kutekeleza mradi wa ujenzi wa meli tatu katika Ziwa Nyasa, mbili kati ya hizo ikiwa ni kwa ajili ya mizigo na moja kwa ajili ya abiria na mizigo. 

Kazi ya ujenzi wa meli hizo ilipewa Kampuni ya Songoro Marine ambayo ni kampuni ya Kitanzania. Meli ya mizigo ya kwanza ambayo imepewa jina la MV Njombe yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kwa wakati mmoja na meli nyingine ya mizigo ya MV Ruvuma nayo ina uwezo wa kubeba tani 1,000 kwa wakati mmoja.

Aidha, kwa upande wa meli ya tatu ya abiria na mizigo ilipewa jina la MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200. Kazi ya ujenzi wa meli tayari imeshakamilika wakati kazi ya ujenzi wa meli mbili za mizigo nayo tayari ilikwishakamilika tangu mwaka 2017.

Manufaa ya meli hizi katika Kanda ya Ziwa Nyasa ni kubwa na nyingi, ikiwa ni pamoja na kuboresha shughuli za usafirishaji na mzunguko wa kibiashara katika maeneo ya Ziwa Nyasa. Kwani uwepo wa meli mbili za mizigo na matarajio ya kuingia kwa meli ya abiria kutarahisisha shughuli za usafirishaji katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Hii ni pamoja na kuboresha hali ya uchumi kwa jamii zinazoishi katika miji ya pembezoni mwa ziwa kwa kuongeza wigo na mwingiliano wa Kibiashara. Aidha, inatarajiwa kuwa uwepo wa meli hizi za abiria utachangia sana katika kuongeza shehena ihudumiwayo katika Bandari za Ziwa Nyasa. 

Manufaa mengine ni kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi wa maeneo ya jirani na Ziwa Nyasa. Wananchi wa Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, mikoa ya pembezoni mwa Ziwa Nyasa na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla wamepata manufaa kutokana na ujenzi wa meli hizi. Moja kati ya manufaa waliyopata ni ajira mbalimbali katika kipindi chote cha ujenzi wa meli hizi.

Faida nyingine iliyopatikana na itakayoendelea kupatikana kutokana na uwepo wa meli hizi ni kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa katika maeneo yanayopitiwa na Ziwa Nyasa. Uwepo wa meli hizi utapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa katika ukanda wa Ziwa Nyasa kwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba usafiri wa majini hasa kwa kutumia meli za kisasa kama hizi ni rahisi ukilinganisha na usafiri/usafirishaji kwa njia ya barabara. 

Mfano, gharama ya kutoa tani moja ya makaa ya mawe kutoka Ngaka hadi Mbeya ni wastani wa fedha za Kitanzania Sh 110,000. Gharama hii ni kubwa ukilinganisha na gharama za usafirishaji kwa njia ya Ziwa Nyasa ambayo inakadiriwa kuwa ni Sh 85,000. 

Aidha, meli hizi zitaboresha usalama wa abiria na mali ziwani, kwani Ziwa Nyasa ni miongoni mwa maziwa yenye mawimbi makubwa (hadi kufikia mita 2.5), hali ambayo ni hatari kwa wasafiri na mizigo inayosafirishwa ziwani kwa kutumia boti na ngarawa. Hivyo ujio wa meli hizi tatu utawaondolea wasafiri hatari (risk) ya kudhurika pindi kunapokuwa na machafuko ziwani. 

Meli hizi pia zinapunguza msongamano wa malori na shehena zinazosafirishwa kwa njia ya barabara. Meli hizi zinatarajiwa kupunguza idadi kubwa ya malori yanayopita barabarani, kwa kuwa mzigo mwingi utakuwa ukipitishwa kwa njia ya majini.

Hali hii itasaidia kupunguza misongamano isiyo ya lazima barabarani, sambamba na kuipunguzia serikali gharama za ukarabati wa mara kwa mara wa barabara zetu. Mfano, meli moja yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo ni sawa na malori 33 yenye uwezo wa kubeba tani 30 kila moja. 

TPA inatekeleza miradi ya upanuzi wa Bandari ya Kiwira. Bandari hii ni lango kuu la usafirisaji wa mizigo katika Ziwa Nyasa, ambapo asilimia zaidi ya 90 ya shehena zinazohudumiwa na Mamlaka katika Ziwa Nyasa hupita katika bandari hii. Bandari ya Kiwira ndiyo bandari muhimu katika upitishaji wa makaa ya mawe kutoka katika Wilaya ya Nyasa na Mbinga zilizopo mkoani Ruvuma, pia bandari hii inatumika kuhudumia mizigo mchanganyiko inayosafirishwa kwa njia ya maji katika ukanda wote wa Ziwa Nyasa. 

Kwa kuzingatia umuhimu wa bandari hii, katika mwaka wa fedha 2018/19 TPA iliamua kutekeleza miradi miwili muhimu ya upanuzi wa Bandari ya Kiwira ili kuboresha ufanisi wa kazi za bandari hii.

Mradi wa kwanza ni ujenzi wa sakafu ngumu (Heavy duty paving). Lengo kuu la mradi huu ni kupanua eneo la kuhifadhi shehena, pia ujenzi huu utaiwezesha Bandari ya Kiwira kuhudumia shehena nyingi zaidi kwa wakati mmoja na kuboresha mzunguko wa meli (ship turnaround time) kwani mzigo wote unaowasili na meli utakuwa ukipakuliwa kwenye yadi na kuruhusu meli kwenda kuchukua mzigo mwingine. 

Mradi wa pili ni ujenzi wa gati mbili (ramps) kwa ajili ya kufunga meli, jengo la ofisi na mgahawa. Lengo kuu la mradi huu ni kuongeza ufanisi wa Bandari ya Kiwira kwa kuiwezesha kuhudumia idadi kubwa ya meli kwa muda mfupi.

Aidha, kukamilika kwa mradi huu kutaiwezesha Bandari ya Kiwira kuhudumia meli tatu kwa wakati mmoja, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo bandari inaweza kuhudumia meli moja tu kwa wakati mmoja.

Aidha, ujenzi huu utaiwezesha Bandari ya Kiwira kuhudumia shehena nyingi zaidi kwa wakati mmoja na kuboresha mzunguko wa meli, kwani hakutakuwa na ucheleweshaji wa meli unaotokana na kusubiri nafasi ya kufunga gatini. 

Pia mradi huu utaongeza usalama kwa meli za Mamlaka zilizopo katika Ziwa Nyasa, kwani meli hizi zitakuwa zikifunga gatini kwa umadhubuti zaidi, hivyo kuziepusha na athari za dhoruba za mawimbi yanayotokea mara kwa mara ziwani. Inakadiriwa kwamba Ziwa Nyasa lina wastani wa mawimbi yenye urefu wa mita 2.5 pindi hali ya hewa inapochafuka. 

Katika mwaka wa fedha 2019/20, Mamlaka inatarajiwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Ndumbi kwa kuweka gati la kudumu, jengo la ofisi, sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia makaa ya mawe sambamba na nyumba ya mtumishi.

Ujenzi huu utaboresha shughuli za uhudumiaji wa shehena ya makaa ya mawe katika bandari hiyo ambapo wastani wa tani 6,000 zinatarajiwa kuhudumiwa kwa mwezi sawa na makusanyo ya Sh milioni 300 kwa mwezi. 

Vilevile serikali imedhamiria kufungua ushoroba wa Mtwara kupitia Bandari ya Mbamba Bay ambapo tayari imeshaweka miundombinu ya barabara hadi Mbinga na inatarajiwa kwamba mpaka kufikia mwaka 2020 kipande cha lami cha kilometa 67 kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay kitakuwa kimekamilika.

Mpango huu wa serikali unakwenda sambamba na upanuzi wa Bandari ya Mbamba Bay, ambapo tayari Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imeanza mchakato wa kutwaa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya bandari.

Kufunguka kwa ushoroba wa Mtwara kutawapunguzia umbali wasafirishaji wa Malawi kwa takriban kilometa 450 kutoka bandarini. Mfano, umbali kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi mji wa Lilogwe ni kilometa 1,700, ila kwa kupitia ushoroba wa Mtwara umbali huo unapungua hadi kufikia kilometa 1,250.

192 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!