Treni, mabehewa SGR ni mitumba

*Ni tofauti na tambo za awali za TRC kuwa wangeleta injini, mabehewa mapya kutoka kiwandani

*Ukarabati, utiaji nakshi mabehewa chakavu haujakamilika; TRC, mzabuni waingia kwenye mgogoro wa malipo

NA MANYERERE JACKTON

DAR ES SALAAM

Injini na mabehewa ya treni vilivyoagizwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa ajili ya reli ya kisasa (SGR) ni mitumba.

Injini hizo mbili na mabehewa 30 vimegharimu euro milioni 28.3; sawa na Sh bilioni 73.74. Hata hivyo, baada ya majadiliano mzabuni alishusha kiasi hicho kwa asilimia 6 (euro milioni 1.698), hivyo gharama halisi ya zabuni kuwa euro milioni 26.602.

Pamoja na mambo mengine, gharama za zabuni hiyo zinahusisha huduma ya vipuri kwa miaka mitatu, mafunzo kwa wafanyakazi wa TRC, majaribio ya injini na mabehewa, ufungaji mifumo ya kamera za usalama, televisheni na viyoyozi.

Malipo ya asilimia 35 yalitakiwa yawe malipo ya awali baada ya TRC ‘kuhakikishiwa’ umiliki wa injini mbili na mabehewa 30. Malipo ya asilimia 40 yalipaswa yafanywe baada ya taratibu za kusafirisha vifaa hivyo kuja nchini kukamilika. Asilimia 20 ya malipo yangefanywa baada ya majaribio na kujiridhisha kuhusu ubora wa injini na mabehewa hayo. Asilimia 5 ya malipo kwa mujibu wa mkataba yalipaswa yafanywe baada ya kumalizika mafunzo kwa wataalamu wazawa na kipindi cha matazamio (warranty).

Taarifa za ujio wa mitumba hiyo zinakinzana na tambo za mara kwa mara za TRC kwamba injini na mabehewa vinavyoletwa ni vipya kutoka kiwandani. JAMHURI limethibitishiwa kuwa injini na mabehewa hayo vina umri wa kati ya miaka 20 na 25.

“Hali hii inafanya vihitaji ukarabati wa hali ya juu pamoja na kuwekwa nakshi ili walau vivutie machoni,” kinasema chanzo chetu.

Kuna madai kwamba injini hizo ni sehemu ya injini moja iliyoletwa na kuibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii kabla ya TRC kujitetea kuwa injini hiyo ni mali ya mkandarasi, Kampuni ya Yapi Merkezi, inayojenga SGR; na imeletwa kwa ajili ya majaribio.

TRC wametumia mwanya na udhaifu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma kununua vifaa hivyo; kwani licha ya serikali kubanwa kisheria kwa kutakiwa kununua vitu vipya, ruhusa maalumu imetolewa kwenye ununuzi wa mitumba ya ndege, meli na treni. 

Mzabuni aliyepewa kazi hiyo kupitia zabuni yenye namba PA/154/HQ/2019-20/G/O1D ni Kampuni ya Eurowagon Demiryolu Ticaret Ve Ltd ya nchini Uturuki. Mkataba huo ulitiwa saini Oktoba 1, 2020. Kwa mujibu wa mkataba, kazi hiyo ilipaswa iwe imekamilika ndani ya miezi tisa, lakini hadi wiki iliyopita shehena hiyo ilikuwa haijakabidhiwa. Kwenye utiaji saini TRC iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wake, Mhandisi Masanja Kadogosa, na kwa upande wa Eurowagon mwakilishi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji, Yalcin Aydemir.

 Nyaraka za kumbukumbu zinaonyesha kuwa mazungumzo ya awali yaliyowezesha kupatikana kwa mzabuni yalianza Juni 25-27, 2020 na baadaye yakahitimishwa kwa kikao cha Julai 1-3 na Julai 15, 2020.

 Waliohudhuria kwa upande wa TRC ni Mhandisi Yusto Goima (Mwenyekiti), Mhandisi Kelvin Kimario (Katibu), Mhandisi Mateshi Tito, Mhandisi Enock Mgonja, Mhandisi Manase Le-Kujanm (TEMESA) na Ramadhan Mbahe (Mwanasheria). Kwa upande wa Eurowagon, waliwakilishwa na Yalcin Aydemir na Mehmet LezginBucak.

 Kwenye mkataba huo, vichwa viwili vya treni gharama yake ni euro milioni 2.422 (Sh bilioni 6); ilhali mabehewa 30 yamegharimu euro milioni 24.18 (Sh bilioni 59.5). Mwishoni mwa wiki iliyopita euro moja ilikuwa sawa na Sh 2,462.

Mzabuni alitakiwa awe amekamilisha kazi hiyo kwa awamu mbili ndani ya miezi tisa. Awamu ya kwanza (miezi mitano) awe ametengeneza, amekarabati na kukamilisha kazi ya injini mbili za treni ya umeme, pia awe ametengeneza mabehewa 12 ya abiria. Awamu ya pili (miezi minne) awe ameshakarabati mabehewa 18 ya abiria.

Kwa mujibu wa mkataba, mzabuni alitakiwa awe amekamilisha kazi Juni 30, mwaka jana, lakini haikuwezekana kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kukwazwa na athari za ugonjwa wa Uviko-19.

Muda huo uliongezwa hadi Februari 28, mwaka huu baada ya makubaliano ya kuuhuisha mkataba yaliyofikiwa na pande zote mbili. Hata hivyo, bado kazi hiyo haikukamilishwa, hivyo kuzifanya pande zote mbili kwenye mkataba huo (TRC na Eurowagon) ziingie kwenye mgogoro.

Habari za uhakika kutoka ndani ya TRC zinasema tayari shirika hilo limeingia kwenye mgogoro na Kampuni ya Eurowagon inayotaka ilipwe fedha kwa kazi ilizokwishafanya. Mkaguzi aliyechaguliwa na TRC (kwa mujibu wa mkataba), alithibitisha kuwa Eurowagon wameshafanya kazi yote kwa asilimia 50.

Julai 26, mwaka jana, TRC kupitia kwa Vincet Tangoh kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu waliiandikia barua Eurowagon wakilalamika kutokamilisha kazi kama ilivyo kwenye mkataba.

Kwa mara nyingine, Februari 10, mwaka huu TRC walimwandikia mzabuni huyo kumkumbusha utekelezaji wa mkataba, na wakatishia kuuvunja endapo angeshindwa kutekeleza yaliyokubaliwa na pande zote mbili.

“Kwa kuwa umeshindwa kutekeleza vipengele vya mkataba, mtoa zabuni chini ya kifungu 156.2 (a) cha mkataba atalazimika kuvunja mkataba. Mtoa zabuni anatoa siku 14 na endapo hakuna kitachofanyika, atalazimika kuvunja mkataba,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Kwa upande wao, Eurowagon wanajitetea kwa kusema kwamba kuchelewa kwao kumaliza kazi kulisababishwa na janga la Uviko-19; lakini pamoja na yote hayo bado walifanikiwa kumaliza kazi kwa asilimia 50. Wanataka walipwe kulingana na kazi ambayo wamekwisha kuifanya.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Eurowagon, Aydemir, katika barua yake ya Mei 5, mwaka huu kwenda kwa Kadogosa anasema kiasi walichokwishapewa ni asilimia 35 pekee, ambacho ni euro 9,310,700 (Sh bilioni 23). Fedha hizo zililipwa Februari 16, mwaka jana.

“Mkataba uliotiwa saini Oktoba mosi, 2020 umevunjwa na TRC kwa hila. TRC ilikumbushwa na Kampuni ya Kitaliano ya RINA ambayo iliteuliwa na mkaguzi wa TRC, Novemba 18, 2021 ilitoa taarifa kwamba Eurowagon Demiryolu Tic. Ltd. Sti. imefanikisha kukamilisha kazi kwa asilimia 50. Taarifa ya RINA inasema wazi kuwa licha ya kuwapo Uviko-19 imefanikiwa kufanya kazi kwa weledi,” wanasema Eurowagon kwenye barua yao.

Eurowagon wanataka walipwe asilimia 15, yaani euro 3,930,300 (Sh bilioni 9.7) ambazo pamoja na zile za awali (Sh bilioni 23) zinafanya malipo stahiki kulingana na kazi iliyokwisha kufanywa ya asilimia 50 ya mkataba wote. Walitoa hadi Mei 13 wawe wamelipwa kiasi hicho cha fedha, vinginevyo wangeshitakiwa katika mahakama za ughaibuni.

Mei 16, mwaka huu Eurowagon walimwandikia Kadogosa barua wakikumbushia barua yao ya awali kuhusu mapunjo wanayodai kutokana na kazi waliyokwisha kufanya kwa mujibu wa mkataba wa zabuni hiyo ya mwaka 2020.

“Katika barua yako ulieleza mambo mawili: kwamba uko tayari kuketi nasi kumaliza mgogoro huu, na pili ofisi yako haipo tayari kulipa deni tunalodai kwa madai kwamba tumechelewesha kazi ya injini mbili za treni na mabehewa 30 ya abiria; na ukaenda mbali zaidi kwa kututaka tukulipe euro 3,471,561 (Sh bilioni 8.546) kama fidia kwa kuchelewesha kazi,” inasema barua ya Eurowagon.

Wao wakasema kwa mujibu wa mkataba, malipo yanatakiwa yafanywe kulingana na kazi inavyokamilika. 

“Desemba 15, 2021, tathmini iliyoletwa kwako na ilisema wazi kwamba kutokana na Uviko-19, kazi iliyofanywa inakidhi matakwa ya mkataba baina yetu. 

“…Tumekamilisha kazi kwa asilimia 50 kama ilivyotakiwa kwenye mkataba, kwa hiyo tunastahili kulipwa euro 3,930,300 sawa na asilimia 15 ambazo ni sehemu iliyokuwa imesalia kwenye malipo ili kukamilisha asilimia 50 kwa mujibu wa mkataba. 

“Tunapenda kukutaarifu kuwa hatukusudii kuendelea na kazi iliyobaki hadi hapo utakapokuwa umetulipa kiasi tunachokudai, na suala hili limalizwe kiungwana kwa manufaa ya pande zote mbili.

“…Kwa maana hiyo, unatakiwa kutulipa kiasi kilichobaki cha euro 3,930,300 ambazo ni asilimia 15 ya sehemu ya kiwango kilichomo kwenye mkataba wetu wa Oktoba 1, 2020… unatakiwa kulipa ndani ya siku nne tangu siku ulipopata majibu haya ya barua yako. Tambua kuwa kushindwa kufanya hivyo ndani ya muda huo, hatutakuwa na njia nyingine ya kufanya isipokuwa kwenda kortinikwa gharama zako,” amesema Aydemir katika barua yake kwa TRC.

Msemaji wa Eurowagon, ameliambia JAMHURI kuwa mkataba wao umekatishwa kwa namna ambayo si ya kiungwana. 

“Sisi tunadai malipo kwa kazi tuliyofanya. Ulimwengu mzima unajua Uviko-19 ulivyoyumbisha shughuli za kiuchumi, lakini sisi tuliweza kufanya kazi kwa asilimia 50. Bado TRC wanaona tumevunja mkataba, hii si haki.”

Mkururugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Kadogosa, ameulizwa na JAMHURI kuhusu mgogoro huu na awali alipinga kuwapo kwa mvutano kati yao na Eurowagon.

“Mgogoro upi tena? Kila jambo ambalo tunafanya ndani ya taasisi liwe ni ujenzi au ununuzi linasimamiwa na mikataba au mkataba. TRC hatuna mgogoro wowote ndugu yangu,” amesema.

Lakini baada ya kuonyeshwa nyaraka zinazoelezea mgogoro huo, akasema: “Si inasomeka (barua yake kwenda kwa Eurowagon) vizuri kabisa; hao ni watu wanatapatapa tu ndugu yangu; hakuna mgogoro hapo. Kama wao walikupa hizo barua ambazo tulishawaandikia kwa mujibu wa mkataba na hawakubaliani, mkataba unawapa haki ya kwenda kwenye mapatanisho au mahakamani.”

Akaulizwa kama tayari mkataba kati ya TRC na Eurowagon umeshavunjwa, Kadogosa anajibu: “Sasa ndugu yangu waliokupa hizo barua waseme, mambo ya ofisi yanabakia mambo ya ofisi, aliyekupa hizo barua muulize.”