Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Katavi

Idara ya Uhamiaji imewakamata wahamiaji haramu 65 raia wa Ethiopia ambao walikuwa wanasafirishwa kwa gari ya kubebea mafuta.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka idara hiyo imesema kuwa wahamiaji hao walikuwa wanasafirishwa kutoka mkoani Mwanza kuelekea Tunduma.

Walikamatwa Jumatatu majira ya mchana katika kizuizi kilichopo katika kijiji cha Kamsisi Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Idara ya uhamiaji imesema kuwa pia watu wanne raia wa Tanzania walikamatwa akiwemo dereva wa gari hilo.

Watu wote hao wanashikiliwa kwa hatua zaidi za kisheria.

Mara kwa mara Tanzania hutumika kama njia ya kupita ya wahamiaji haramu kutoka Eritrea na Ethiopia ambao wengi wao huelekea Afrika Kusini au Ulaya.

Kwa wale wanaoshindwa kufanikiwa safari yao huishia kukamatwa, wengine hutelekezwa na madereva wakiwa wamekufa au kuwa na hali mbaya kiafya.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), linakadiria kuwa tangu mwaka 2014 karibu wahamiaji 50,000 wamekufa au kutoweka wakijaribu kufika nchi kama Marekani au Umoja wa Ulaya. Shirika hilo linaamini kwamba idadi halisi ya watu wanaokufa au kutoweka huenda ikawa juu zaidi.

Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mlele Majid Mwanga amesema kuwa wahamiaji hao wamekamatwa Kijiji cha Kamsisi kilichopo Kata ya Kamsisi kwenye kizuizi geti la maliasili  majira ya saa 5, Agosti 14,2023 ambapo Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na askari wa huduma za misitu TFS na watumishi wa Halmashauri walioko kwenye geti hilo na wale wa kwenye mizani ya Kamsisi  ambao wamesaidia kukamatwa kwa lori lilolokuwa limebeba  wahamiaji hao.

 Walikuwa wanasafiri kwa gari kubwa lori  la mafuta lenye namba za usajili T.952 DFB ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva anayejulikana kwa Msadick Mohamed Msomolo Mkazi wa  Mwanza, akiwa na mwenzake  mkazi wa Kihonda Mkoa wa Morogoro.

Gari hilo lilikuwa likitokea Mkoa wa Mwanza kuelekea Tunduma Mkoa wa Songwe kupitia Sumbawanga Mkoa wa Rukwa,

Wahamiaji hao   walibebwa ndani ya gari hilo kutoka eneo la Kisese Mkoa wa Mwanza na walikuwa wakipelekwa Tunduma  Mkoa wa Songwe kwa safari ya kwenda nje ya nchi.

Kukamatwa kwa wahamiaji hao mkuu wa wilaya amepongeza moyo wa uzalendo ulioneshwa na watumishi wa Idara ya uhamiaji, Wakala wa Misitu TFS ,watumishi wa wakala wa barabara upande wa mizani  na watumishi wa Halmashauri waliokuwa kwenye geti la Kamsisi waliosaidia kufanikisha kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu

By Jamhuri