Uhuru, Mapinduzi na Muungano ni muhimu kwetu (2)

Katika miaka 58 ya Uhuru na miaka 56 ya Mapinduzi hamna kilichofanyika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii Watanzania. Aidha, katika Muungano hamna faida kwa Wazanzibari, bali kuna mafanikio kwa Watanganyika. Kauli hizi zina ukakasi na mzizimo kwa Watanzania.

Maneno haya yanapotolewa na kiongozi wa aina yeyote Tanzania, na Watanzania fulani fulani wakayabeba na bila kutafakari kwa kina wakaimba kila mtaa, ni dhahiri wote wana jambo lao, ambalo kwao lina manufaa na kwa taifa lina hasara na chuki.

Ninapowasikiliza kwa nyimbo zao hizi, huwa ninahuzunika, ninasikitishwa na kujiuliza, ni kweli Tanzania hamna maendeleo yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 58? Au ni bashrafu kusikilizwa kabla ya maudhui ya wimbo kutamkwa na kuonyesha njia ambamo mwimbaji atapitia?

Viongozi hawa na wafuasi wao wanaonyesha dalili kwamba hawana mema kwa taifa letu. Kitabia ni watu wenye dharau, ujinga na kiburi. Tabia tatu hizi zinapomvaa mtu hutokwa na sifa ya utu, maarifa ya kupima madhila na majira kupata majawabu sahihi na kuyazungumza kwa jamii.

Ni dhahiri, wanayo macho lakini hawaoni. Wanayo masikio bado hawasikii. Lililo shahiri kwao ni gere, choyo na wivu, kwa viongozi wanaoleta maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi. Tuwazungumze na tuwaambie bayana waache tabia ya lila na fila na wabebe tabia ya msumeno.

Hata hivyo, ninaona iko haja kwa Watanzania na wataalamu wa mipango ya maendeleo nchini kupiga mbizi au kuingia msambweni kutafuta haiba ya Tanzania na kuangalia kama kweli hakuna maendeleo, ili kupata majawabu ya kukubali ama kukataa nyimbo zao kuimbwa hadharani na vichochoroni.

Kabla ya kupiga mbizi au kuingia msambweni ni busara kwako na kwangu tukaangalia mtunzi wa nyimbo na waimbaji ni wenzetu au ndio katika wale. Wale wanayo tabia kama ya ng’ombe kutoa ulimi kinywani mwake na kuuingiza puani mwake na kuurudisha kinywani.

Tangu tupate Uhuru, tufanye Mapinduzi na kuuweka Muungano wetu, wapo viongozi na wafuasi wao wachache ambao usiku na mchana wanapanga mipango kuhujumu uchumi wa nchi, kufanya ufisadi, kutusaliti na kutoa rushwa kuwarubuni Watanzania wasifanye shughuli za maendeleo. Leo wanaimba hamna kilichofanyika!

Pamoja na vitimbi na visa vyote hivi wafanyavyo, na kukubali wao ni wasaliti na vibaraka katika nchi yetu, na kujionea ufahari kwa mara ya pili kuwa watumwa, kukubali kuwa watupu wa fikra, na kutii wao ni dhalili mbele ya mabeberu, sisi Watanzania huru tunapiga hatua kubwa ya maendeleo.

Kuwa watu huru wenye uamuzi wa kujiongoza na kujitawala wenyewe, kushinda hila zote za udhalilishaji, kukataa unyonge, kutunza na kulinda mali na rasilimali zetu, kujenga taifa imara lenye watu wapatao milioni 55 kutoka milioni 9.5 wakati wa Uhuru na Mapinduzi ni maendeleo makubwa sana.

Kujenga sifa duniani kwamba Watanzania tunadumisha amani na utulivu, kuimarisha Muungano wetu kwa miaka 56 kwa amani, kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia katika uchumi na siasa na kuonyesha wazi tabia yetu ya ukarimu kwa wageni wetu ni maendeleo.

Mabalozi nchini na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kutambua na kuthamini miradi yetu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kupunguza umaskini ni dhahiri shahiri wanaona hatua kwa hatua jitihada tunazofanya za kujiletea maendeleo ya watu.

Uhuru, Mapinduzi na Muungano vimetuwezesha Watanzania kushirikiana na kushikamana katika kupanga mipango yetu ya maendeleo. Kila sekta ya jamii na uchumi imeboreka, imepanuka na imeimarika katika kutoa huduma ya maji, afya na elimu.

Ni kweli ni vigumu kuzuia kinywa cha mtu kutoa maneno ambayo tayari yamepangwa kichwani mwake. Utaratibu huu unawezekana kudhibitiwa iwapo tu ukweli utatawala vinywa vya watu, na nafsi zitaacha choyo, na uadilifu kutamalaki katika nyoyo zetu chini ya misingi na maana ya Uhuru, Mapinduzi na Muungano.