Ummy: Rais Samia amedhamiria kuleta mapinduzi viwanda vya dawa na vifaa tiba

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuleta mapinduzi sekta ya viwanda hususani viwanda vya dawa na vifaa tiba.

Amesema katika hatua hiyo, Rais Dk. Samia anaendelea kutoa fedha kwa ajili ya uwekezaji sekta ya viwanda na miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa awamu ya tano inatekelezwa.

Waziri Ummy amesema hayo jana Mkoani Njombe wakati wa ukaguzi wa uzalishaji wa kiwanda cha mipira ya mikono (gloves) kilichopo Idofi Mkoani Njombe kinachosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD) ambacho keshokutwa kinatarajia kuwekwa jiwe la misingi na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.

Alisema ujenzi na uzalishaji wa kiwanda cha mipira ya mikono Idofi kinachosimamiwa na MSD unaridhisha na kukidhi mahitaji.

Aliongeza kuwa uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba unaofanywa na serikali unaenda kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi na matumizi ya fedha za kigeni.

Alieleza kuwa, katika hatua ya uwekezaji wa kiwanda hicho, Rais Dk. Samia alikuta kikiwa asilimia 30 na sasa ni asilimia 90.

“Lengo la serikali ya Rais Dk. Samia ni kufikia asilimia 50 kutoka asilimia 15 iliyopo sasa katika ununuzi wa bidhaa za afya ndani ya nchi kufikia mwaka 2030,”alisema.

Alisema kwasasa vifaa vya afya kwa asilimia 85 tunanunua kutoka nje na unaponunua kuna changamoto ikiwemo kusubiri kwa miezi tisa bidhaa kufika hali inayosababisha uhaba wa dawa na kuongezeka matumizi ya fedha za kigeni.

Waziri Ummy alisisitiza kwa sasa kuna viwanda 30 vya dawa na vifaa tiba vya ndani na kati ya hivyo 11 vinafanya kazi.

Alithibitisha kuwa tayari serikali imetoa zaidi ya sh Bilioni 11 ya uendelezaji wa kiwanda hicho na kudhamiri kuongeza uzalishaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.

“Nipongeze sana bodi ya MSD hapa tunazungumzia bidhaa za afya za watu lazima kujiridhidhisha wamefanya hivyo na kiwanda kiko vizuri ambapo tutakifungua kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa,”alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, alisema kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa awali na kinatararajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema kiwanda cha mipira ya mikono (gloves) Idofi hadi kikamilike kitagharimu sh. bilioni 22.5, baada ya kukamilika kwa ujenzi na ufungaji wa mitambo, kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mipira ya mikono 20,000 kwa saa sawa na jozi(pairs) 10,000 na hivyo kufanya uzalishaji wa takribani jozi 86,400,000 kwa mwaka.

“Hii ni sawa na asilimia 83.4 ya makadirio ya mahitaji ya mipira ya mikono nchini ya jozi milioni 104 kwa mujibu maoteo ya uhitaji ya bidhaa za gloves nchini kwa mwaka 2023/2024,”alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka alisema, Rais Dk. Samia amefanya mabadiliko makubwa katika kiwanda hicho na amedhamiria kuona uzalishaji wake unakuwa na tija kwa Watanzania na hasa wananchi wa Njombe ambao wameanza kunufaika na fursa zilizopo hususani kupata kipaumbele katika ajira.