Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umezielekeza Benki na taasisi nyingine za kifedha Pamoja na sekta binafsi kushirikiana moja kwa moja na Wizara ya kilimo katika kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata mitaji, masoko na teknolojia za kisasa katika kushiriki kilimo biashara.

Agizo hilo limetolewa leo Mei 24,2023 Jijini hapa na Katibu wa Idara ya uhamasishaji na Chipukizi UVCCM Edna Lameck wakati akitoa taarifa ya tathmini ya ziara ya Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mohmed Kawaida katika ziara ya ukaguzi wa mradi wa vijana (BBT).

Aidha imeshauri hamshari zote nchini zinazoshiriki katika sekta ya kilimo kutenga ardhi kwa ajili ya vijana wa BBT na vijana wote nchini na kushikiana na wizara ya kilimo kuandaa mashamba makubwa ya Pamoja ambayo tayari Dk.Samia amepeleka Zaidi ya sh.bilioni 361 kwa ajili ya miundombinu ya umwagiliaji.

Amefafanua kuwa ili jambo hilo liweze kufanikiwa Wizara ya Kilimo inapaswa kushirikiana na Wizara ya Elimu kuanza mchakato wa kuwa na Vyuo Vikuu vya Kilimo vitakavyotoa shahada zitakazoendana na mazingira.

Amesema kuanzishwa kwa vyuo hivyo kutasogeza utaalamu karibu na wakulima na kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

“Mnamo tarehe 17 April 2023 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana CCM ndugu Mohamedi Ally Kawaida alifanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama katika mradi wa vijana na wanawake wa Building Better Tomorrow Youth Initiatives in Agribusiness (BBT) katika vituo atamizi 9 kati ya 13 vilivyo katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Kagera, Kigoma na Tabora” amesema.

Ameeleza kuwa mradi huo umeteua vijana 812 katika awamu hii ya kwanza ambapo vijana wa kiume ni 530 na wa kike 282, kwa sasa wizara inaendelea na dirisha la pili la vijana watakaoshiriki katika mnyororo wa thamani .

“UVCCM inaona BBT ni program inayolenga kuwezesha na kuongeza Zaidi ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo biashara ili kuwapataia ajira, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa Pamoja na kuinua hali ya Maisha ya jamii ya watanzania,”amesisitiza.

Mbali na hayo amesema kwa sasa Serikali ina mawajabu ya vijana kushindwa kumiliki ardhi kwa ajili ya kilimo biashara, kukosa ujuzi masoko, mitazamo hasi na utegemezi wa kilimo cha mvua ambacho kwa muda mrefu kimeifanya sekta ya kilimo kuwa mwendo wa kobe.

“Utekelezaji wa lengo la miaka minane ya BBT la kuwa na angalau na biashara moja ya kilimo yenye faida na endelevu inayoongozwa na vijana katika vijiji 12,000 inatarajia kutengeneza ajira Zaidi ya milioni 3 ifikapo 2025/2030,”amesema

By Jamhuri