Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiambia dunia kuwa uwekezaji wa kweli katika nishati ni kuwekeza katika nishati safi ya kupikia barani Afrika.

Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati anahutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Korea na Afrika unaofanyika Seoul, Korea tarehe 04 na 05 Juni 2024.

Rais Samia amesisitiza umuhimu wa wadau kuongeza ushrikiano ili kuharakisha utekelezaji wa agenda hiyo ambayo sio tu itapunguza tatizo la uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa misitu, bali itapunguza pia vifo vinavyotokana na magaonjwa yanayotokana na matatizo ya upumuaji.

Rais Samia alisema kuwa uwekezaji katika nishati salama barani Afrika utaongeza fursa za kiuchumi kwa kubuni miradi itakayo kuwa ufumbuzi wa kupata nishati safi ya kupikia.

Rais Samia amemalizia kwa kusema kuwa yeye na Rais wa Benki ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina wapo katika zoezi la kutafuta fedha za kutekeleza agenda hiyo na kutoa wito kwa Korea kuunga mkono zoezi hilo.

Mkutano wa Korea-Afrika ni mara ya kwanza kufanyika kwa ngazi ya Wakuu wa Nchi na unajadili maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Korea na Afrika, kuhamasisha mageuzi ya viwanda na miundombinu ya kidigitali hasa katika sekta ya kilimo na uvuvi na kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazozikabili dunia hasa katika uhaulishaji wa teknolojia ya miradi ya kilimo. (agricultural technology transfer projects).