Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Vilio na simanzi vimetawala  leo wakati wa kuuaga mwili wa aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Barabara ( TANROADS ), Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Mlima  Felix Ngaile( 55) aliyefariki jana wakati akikimbia.

Marehenu alifariki ghafla jana Januari 12, 2024 baada ya kupata mshituko wa moyo wakati akikimbia mbio za hisani za Km 5 zilizoandaliwa na Shirika lilisilo la kiserikali la Wiloles Foundation kwa ajili ya kuchagia fedha za kununua  vifaa tiba ili kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (Njiti).

Akiongoza mamia ya waombolezaji ambao walijitokeza kwa wingi kwenye ibada ya mazishi  iliyofanyika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea na kuhudhuliwa na viongozi mbali mmbali wa chama na serikali, wananchi, wakandarasi, watumishi wa TANROADS na TARURA,  Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilman Kapenjama Ndile ambaye alimwakilisha mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amesema kuwa marehemu amefariki kutokana na mshituko wa moyo (BP) .

“Kwa mujibu wa taarifa za madktari marehemu alipatwa na mshtuko wa moyo wakati akikimbia na alikimbizwa hospitali na madaktari walifanya kila jitihada lakini ilishindikana” amesema.

DC Ndile amesema, marehemu alikuwa na dhamila kubwa ya kuchangia matibabu ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda mkoani lakini amepatwa na mauti  wakati akitimiza adhima ya kuhakikisha anashiriki  mbio za hisani kama alivyokuwa ameahidi.

“Kifo kimekatili adhma yake kwa jinsi alivyoondoka ndugu yetu,kwani wapo wanaoondoka ghafla kama mhandisi Ngaile na wapo wanaougua na kulazwa na taarifa za kifo zinapotokea tunasema ameteseka sana tumuache apumzike.

“Hatusemi  kifo kama hicho hakiuzunishi, tofauti na hiki kinachotokea ghafla kinaumiza zaidi  kwani kila mmoja ameandikiwa namna ya kifo chake kwani wapo wataokufa wakiwa safarini, kazini, nyumbani, wamekaa, wakitembeaa, wakikimbia na hata nyumba za wageni vyote ni vifo na vinaumiza”amesema.

Akiongoza Ibada hiyo Paroko wa Jimbo Kuu Songea, Padri Daniel Oteno,  amewataka waumini watambue kuwa maisha ni mtihani wajiandae endepo marehemu Felix angejua kuwa kwenye mazoezi yake ndio ingekuwa mwisho wake angewaaga marafiki zake kuwa hatorudi lakini tutambue maisha ni kama maua asubuhi yanachanua jioni yananyaukaa.

Padri Oteno amewataka watumishi kwenye nafasi zao kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja  na  kujenga tabia ya kumtegemea Mungu kwenye kila kitu wanachofanya ikiwa ni pamoja na kusali zaidi ili kujiandaa kwani maisha  ni mtihani.

“Tujiandae kwa kusali pia wafanyakazi  wachukue kazi zao kama daraja la kwenda mbinguni na siyo kutumia kazi zao kama mwisho wao na wafanye kazi zao kwa kutengeneza barabara kwa ajili utukufu wa kwenda mbinguni” amesema.

Akisoma wasifu wa marehemu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Suleiman  Bishanga  ambaye aliwawakilisha mameneja wa TANROADS nchini  amesema, marehemu alizaliwa Novemba 9,1968 amebahatika kufanya kazi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Mara, Kilimanjaro na  hadi anapatwa mauti alikuwa ni Meneja wa Mkoa wa Ruvuma ambapo alilipoti Oktoba 2023  na ameacha mjane na watoto  watatu , atakumbukwa kwa uhodari wake na pengo lake ni gumu kuzibika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakandarasi Mkoa wa Ruvuma, Charles  Mhagama amesema amepokea kifo hicho kwa uchungu mkubwa wanamuachia Mungu kwani alikuwa msaada kwa wakandarasi  na alitatua kero zao kwa wakati muafaka.

“Kifo sawa na mtego ni vema kucheki afya mara kwa mara na tutende mema kama ambavyo  marehemu alikuwa akifanya ili hata muda wa kuondoka duniani ukifika tukumbukwe kwa mema kama Mhandisi Ngaile,”amesema Mhagama.

Mhandisi  Roman Mbukwini Msimamizi wa kitengo cha Matengenezo amesema wanasikitika kumpoteza meneja huyo kwani alikuwa na ushirikiano mzuri katika kufanikisha jambo kwa uharaka.

“Tumefanya naye kazi vizuri  na amekaa miezi minne Songea lakini alikuwa mfano mzuri katika utendajikazi, ” amesema.

Marehemu anatarajia kusafiri leo Januari 13, 2024 kwenda Shinyanga wilayani Kahama kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika Jumanne.

Amesema kuwa marehemu alikuwa ni zaidi ya mwalimu, zaidi ya baba na kiongozi  kwa watumishi  wenzake.

Hata hivyo ameshauri wanapoandaa mashindano ya riadha yoyote ni vyema kwanza kwa washukiri kupimwa afya zao hasa wenye umri mkubwa ili kuweza  kujua kama wanamatatizo.

Mkurugenzi  wa shirika lisilo la kiserikali  Wiloles Foundation  Geofrey Mdede  ametoa pole kwa familia na wafanyakazi  wa TANROADS walikua naye nusu saa kabla ya kifo chake katika uwanja wa Majimaji akishiriki mbio za Km 5 na baada ya nusu saa akakutwa na mauti kwani tukio hilo limewashtua sana.

Lengo la Marathon  hiyo ilikua ni kuchangia fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kuokoa maisha ya  watoto waliozaliwa kabla ya muda (Njiti) hivyo watakabidhi medali kwani marehemu alikuwa shujaa wao.