DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Wafaransa wanatamka ‘La Norme’. Wareno wanatamka ‘Pradao’. Wahispania wanatamka ‘El standard’. Sisi Waswahili tunatamka ‘Kiwango’. Ndiyo ni kiwango!

Mataifa ya Afrika Mashariki ambayo wakazi wake wengi ni wenye asili ya Kiarabu, ni mataifa makubwa katika soka la Afrika.

Hawa jamaa wametawala soka la Afrika kwa muda mrefu na huenda wakaendelea kulitawala.

Hivi karibuni Waarabu hawa wametuonyesha mahali ambapo wao wapo na sisi tulipo. Miezi kadhaa iliyopita, au tuseme, wakati wa msimu wa usajili mwaka jana, wakubwa hawa waliamua kugawana nyota waliong’aa katika soka la Tanzania.

Mmoja wa nyota hao akaondoka nchini na kwenda zake Morocco. Nyota mwingine naye akatimka na kwenda Misri. Wote wamekwenda huko kusaka malisho mema zaidi. 

Morocco na Misri ni mataifa ya Afrika ambayo wakazi wake ni wenye asili ya Kiarabu. Ni Waarabu.

Hata hivyo, ndani ya miezi mitano tu, mmoja kati ya nyota hawa ninaowazungumzia leo, akarudi Tanzania, mwingine yupo yupo tu huko; ‘anajitafuta’ lakini ‘hajajipata’.

Nieleweke kuwa ninawazungumzia wanasoka wawili waliotamba nchini wakiwa na Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Claotus Chota Chama na Luis Jose Miquissone.

Chama amesharudi Tanzania na anaitumikia klabu yake ya zamani; Simba.

Kuna watu, hasa mashabiki wanaofuatilia soka kwa umakini, wanazishangaa ‘namba’ za Chama tangu atue nchini katika usajili wa dirisha dogo Januari mwaka huu na kuhoji; imekuwaje kiwango hiki hajakionyesha kule alikokuwa kwa Waarabu yaani Morocco? 

Jibu lake ni jepesi sana. Soka letu hapa Tanzania ni laini, tofauti na kule Morocco alikokwenda kusaka mkate mnono zaidi.

Kwa mashabiki wengi, kipaji alichonacho Chama walitarajia kuwa Morroco ingekuwa kama njia yake ya kwenda juu zaidi. Kwamba angepita tu kule.

Hali imekuwa tofauti. Badala yake ndani ya Morocco Chama akawa mchezaji wa kawaida tu. 

Kwa miezi aliyokaa huko akajikuta akiwa benchi kwa muda mwingi tofauti na matarajio yake na yetu pia. Kwa kusema ukweli hili halikutokea kwa bahati mbaya. 

Ukweli ni kwamba kuna sehemu wenzetu wapo ambako sisi hatupo. Bado hatujafika huko.

Soka letu linatudanganya katika vitu vingi. Mchezaji aliyeshindwa sehemu nyingine ni rahisi kuwa nyota mkubwa akija Tanzania. Bangala ni mmoja wa wachezaji hao. 

Bangala alikuwa na kipindi kigumu Morocco, lakini ndani ya Tanzania, amegeuka kuwa malaika wa ardhini. Nini utawaambia manazi wa Yanga juu ya Bangala? Zaidi utaambulia matusi mfululizo.

Alichokutana nacho Chama kule Morocco na anachokipitia ‘Konde Boy’ huko Misri ni kuonyesha jinsi gani soka letu lilivyokuwa chini, licha ya uwekezaji mkubwa ambao umeanza kuwekwa na matajiri.

Huwa najiuliza, kama hawa kina Chama na Konde Boy tuliokuwa tunawaimba vinywani wameonekana wachezaji wa kawaida, vipi kijana wa Kitanzania anayechezea Mbeya City?

Chama na Konde Boy wametuachia maswali magumu sana. Ndani ya Tanzania hawa walikuwa mastaa wakubwa. Maisha yamekuwa tofauti walivyohamia timu nyingine za nje. 

Chama na Konde Boy wangeweza kuwa mastaa wakubwa kama wangehamia nchi za jirani. Zambia, Kenya. Hawa tunafanana nao vitu vingi, lakini wale Waarabu wametuacha mbali. Mbali mno.

Unapoona timu za Kitanzania zimekwenda kucheza Uarabuni na kufungwa idadi kubwa ya mabao, usishituke na kuamini katika figisu, kiwanjani Waarabu ni hatari. Walichotuonyesha kwa Chama na Konde Boy ni ushahidi tosha.

By Jamhuri