Brigedi ya Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO) inayolinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, imewadhibiti waasi wa kundi la March 23 (M23). Brigedi hiyo inayojulikana kwa kifupi kama FIB, inaongozwa na Mtanzania, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa. Kwa sasa imelidhibiti eneo la Goma.

Brigedia Jenerali Mwakibolwa amesema ingawa operesheni ya kuwafurusha waasi hao haijaanza rasmi, hiyo haina maana kuwa wakae tu bila kuwalinda wananchi dhidi ya waasi.

 

Kamanda huyo ametoa kauli hiyo baada ya kuwapo kiu ya muda mrefu miongoni mwa wananchi wa mashariki mwa DRC, wanaotaka kuona waasi wakidhibitiwa na kumalizwa kabisa kwa matukio ya mauaji yanayofanywa na M23 na makundi mengine ya waasi.

 

Brigedia Jenerali Mwakibolwa amesema operesheni haijaanza rasmi kwa kuwa bado wapiganaji wanapewa mazoezi ya nguvu yatakayowawezesha kukabiliana na waasi.

 

Pia amesema bado wanajifunza mazingira, na kwamba wamekuwa wakifanya doria katika eneo la MONUSCO la Kivu ya Kaskazini kwa ajili ya kuilinda Goma na viunga vyake.

 

“Alimradi FIB tupo hapa, Goma haitaangukia tena kwenye mikono ya waasi. Ndiyo maana brigedi inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kunakuwa na doria kwa ajili ya kuilinda Goma na viunga vyake,” amesema na kuongeza kwamba brigedi itakuwa kamili kikazi baada ya askari wote, wakiwamo wa Malawi, kuwasili.

 

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mwakibolwa, asilimia 75 ya askari wote wanaotakiwa kushiriki kwenye brigedi hiyo, wameshawasili Goma. Brigedi itakapotimia itakuwa na askari 3,096.

 

Amesema baada ya kuanza rasmi kwa operesheni, vyombo vya habari vitapewa taarifa mara kwa mara ili walimwengu waweze kujua kinachoendelea.

 

Amesema kwa kuwa shughuli zao za kijeshi wanazifanya chini ya sura ya 7 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, lengo la awali ni kuingilia kati pale inapotakikana, kutuliza na kuwanyang’anya silaha waasi wa makundi yote, likiwamo la M23.

 

Alipoulizwa kama M23 kweli wamemteka askari wa FIB Mtanzania anayedaiwa kushirikiana na kundi la FDLR linaloipinga Serikali ya Rwanda, Brigedia Jenerali Mwakibolwa alisema hizo ni propaganda tu, na kwamba FIB hawapo DRC kivita, bali kuyapoka silaha makundi yote ya waasi na watu wanaozimiliki kinyume cha sheria.

 

Kuhusu madai kwamba FIB inajiandaa kuivamia Rwanda, kamanda huyo amesema, “Rwanda inajua kuwa FIB ipo hapa (Mashariki mwa DRC) kwa ajili ya kuleta amani, na hakuna mpango wala nia ya kuishambulia Rwanda. Tupo hapa kwa ajili ya operesheni ya DRC na siyo Rwanda.”

 

Kamanda wa DRC ajiunga M23

Kanali wa Jeshi la DRC, akiwa na wanajeshi wengine 30 wa Serikali, wameasi na kujiunga na kundi la M23, Jeshi la DRC limethibitisha.

 

Kanali Richard Bisamza aliasi wiki iliyopita, amethibitisha Msemaji wa Jeshi la DRC, Luteni Kanali Olivier Hamuli.

 

“Uamuzi huo si wa kushangaza hata kidogo, hasa kutokana na kabila lake.

 

“Kuondoka kwake hakuwezi kuathiri jeshi letu. Tunapenda kuwa na jeshi lisilokuwa na vibaraka,” amesema Hamuli.

 

Bisamza, ambaye ni Mtutsi, alitakiwa kusafiri kutoka kambini kwake Jimbo la Kivu Kaskazini kwenda Kinshasa, badala yake aliingia msituni na kuungana na waasi wa M23.

 

Hamuli amemshutumu Bisamza kwa kujiunga na M23 ambao ni Watutsi wanaohusishwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda. Umoja wa Mataifa unazituhumu nchi hizo mbili kwa kuwaunga mkono M23.

 

Propaganda za M23

Waasi wa M23 wameendelea kuweweseka tangu walipotambua kuwa brigedi iliyopelekwa DRC inaongozwa na Mtanzania.

 

Kitisho cha kwanza kilikuwa barua waliyoipeleka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakisema msimamo wa Tanzania kupeleka majeshi DRC kupambana na M23 ungeleta kilio kwa Watanzania.

 

Hata hivyo, Tanzania, kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ilipuuza kitisho hicho.

 

Baada ya hapo wameendelea na vitimbi mbalimbali, na cha karibuni kabisa ni cha kuweka nakala ya hati ya kusafiria ya kijana Mtanzania, wakidai ni askari wa Tanzania aliyekamatwa akishiriki mapambano kwa upande wa waasi wa FDLR wanaoipinga Serikali ya Rwanda. Wakadai kuwa mwanajeshi huyo alikamatwa akiwa na bunduki aina ya AK47 yenye namba 1372.

 

Kwenye mtandao wa M23 wa Facebook, kuliwekwa nakala ya hati hiyo na kuambatanisha na maneno yaliyoandikwa kwa Kiswahili ‘kibovu’.

 

Ilisomeka, “Leo FDLR zikiongozwa na askari toka Tanzania zilivamiya Positions zetu pale Kinyadonyi Na Nkwenda huko Rutshuru. Zilikuta Vijana wanazisubiri, walizicapa na kuzikimbiza alafu zikaaca Askari wa Tanzania Nyuma tukamunasa, ivi tuko naye tuko na mupa cayi na mukate anywe. Serikali ya tanzania isiwe na hofu hatutamufanya kitu, tutamucunga muzuri. sisi hatuko kama wale wa criminals wa FARDC ambao wanatukanaka hata maiti, na wenye Wanabakaka watoto wa myaka sita, sisi ni jeshi la Mungu. Kesho mutaona Video yake, Cliquer apa uone passport ya ule askari ya tanzania ambaye tulikamata”

 

Hata hivyo, mamlaka nchini Tanzania zimekanusha kutekwa kwa askari wake, kauli ambayo imeungwa mkono na Kiongozi wa Brigedi ya FIB, Brigedia Jenerali Mwakibolwa.

By Jamhuri