Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya utalii wa ndani wa kutembelea  msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo  Kisarawe mkoani Pwani.

Akizungumzia kuhusu utalii huo Mkurugenzi Mtendaji  wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema wafanyakazi wa Taasisi hiyo  siku ya Jumamosi waliamua kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha utalii na kwenda kufanya utalii wa ndani katika msitu huo.

Dkt. Kisenge alisema wafanyakazi wa JKCI wanafanya kazi katika mazingira ya huruma ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo mbalimbali kwa kufanya kwao utalii katika msitu huo kumewafanya wajifunze vitu vingine vipya tofauti na vile wanavyokutana navyo kazini pamoja na  kujiburudisha.

“Tumewaleta wafanyakazi wetu kutalii katika msitu huu na kuona mazingira tofauti  na yale waliyopo kila siku  ya kuwahudumia wagonjwa kwa kufanya hivi kutawapa ari mpya  ya kufanya kazi pamoja na kutangaza utalii uliopo kwa wagonjwa tunaowahudumia kwani Taasisi yetu ina wahudumia wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi “, amesema Dkt. Kisenge.

Muongoza Watalii kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Omary Sharif  akiwaeleza Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) aina ya vivutio vilivyopo ndani ya  msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo  Kisarawe mkoani Pwani wakati wafanyakazi hao walipofanya utalii wa ndani mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa upande wake muongoza watalii kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Magdalena Lukumay alisema siku ya Jumamosi waliwapokea watalii wa ndani kutoka  JKCI ambao walitembelea msitu huo na kuona vivutio mbalimbali vilivyopo.

Magdalena alisema ni mara chache wanapokea kundi kubwa lenye watalii wengi wa ndani kama ilivyotokea kwa JKCI na kuziomba Taasisi nyingine za Serikali na zisizo za Serikali kuiga mfano huo na kuwapeleka wafanyakazi wao kufanya utalii wa ndani katika msitu huo.

“Katika msitu huu wa mazingira asilia wenyeji waliopo ni kabila la Wazaramo, kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika hapa hii ikiwa ni pamoja na ngoma za asili, matambiko yanayofanyika katika mapango ya mzimu wa Mavoga na vyakula vya asili”, alisema Magdalena.

Nao wafanyakazi wa JKCI ambao walitembelea msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi walishukuru kwa nafasi waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujifunza vitu vipya ambavyo hawakuwa wanavifahamu.

Theresia Marombe ambaye  ni Afisa Muuguzi wa JKCI  alisema amefurahi kutembelea msitu huo na ni mara yake ya kwanza kufika mahali hapo amefurahi zaidi kuona wafanyakazi wote wamekaa pamoja katika mazingira ya asili na kujifunza mambo mbalimbali.

“Kuna umuhimu wa watanzania kutenga muda wa kutembelea  vivutio vya utalii tulivyonavyo na kuona vitu vya asili , kuja hapa ni mara yangu ya  kwanza nitawaambia na wenzangu waje hapa kuona miti, popo na  ndege wa asili waliopo hapa”, alisema Theresia.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika lango la kuingia kwenye msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo  Kisarawe mkoani Pwani walipotembelea msitu huo hivi karibuni kwaajili ya  kufanya utalii wa ndani na kujionea vivutio vilivyopo katika msitu huo.

“Ninashukuru  kupata nafasi ya kutembelea msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi nimeona vitu ambavyo mjini havipo lakini hapa vipo, ninatoa wito kwa watanzania wenzangu wafanye utalii wa ndani kama huu tulioufanya siku ya leo na kuona vitu vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu ametujalia Watanzania kuwa navyo”,  alisema Herry Magwaza ambaye ni Mtunza Kumbukumbu wa JKCI.

Wakiwa katika msitu huo wafanyakazi hao walipata nafasi ya kutembelea  maeneo mbalimbali  ikiwa ni pamoja na bwawa la Minaki lenye kina cha  mita nane na urefu wa kilomita 1.2, mapango ya popo, pango la mzimu wa Mavoga, kupanda mlima wenye urefu wa kilomita 1.5 kwa kutumia kamba pamoja na kuona miti ya asili , ndege, vipepeo na panzi wenye bendera ya taifa.

Muongoza Watalii kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Peter Masome akiwaeleza Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) aina ya miti ya asili iliyopo ndani ya  msitu wa mazingira asilia Pugu Kazimzumbwi uliopo  Kisarawe mkoani Pwani wakati wafanyakazi hao walipofanya utalii wa ndani hivi karibuni katika msitu huo

By Jamhuri