NMB Foundation imetoa wito kwa wahitimu wa Kidato cha Sita mwaka 2026 wenye sifa kuwasilisha maombi ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship kabla ya dirisha kufungwa Ijumaa, Septemba 18, 2026.
Awamu hii imetengewa Sh bilioni 1 kufadhili vijana 50 wenye ufaulu wa Daraja la Kwanza wa pointi tatu hadi tano, wanaotoka familia zenye uwezo mdogo na wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu nchini.
Ufadhili utajumuisha ada na tozo za chuo, fedha za kujikimu, gharama za mafunzo kwa vitendo pamoja na kompyuta mpakato. Wanufaika pia watapata malezi elekezi na maandalizi ya kuingia katika soko la ajira.
Maombi yote yanaendelea kupokewa kupitia tovuti ya NMB Foundation, foundation.nmbbank.co.tz, hadi tarehe 18 Septemba 2026. Wazazi, walezi, walimu na viongozi wa jamii wameombwa kuwafikishia taarifa vijana wenye sifa, hasa walioko vijijini.




