- Programu ya Loyalty yawatoa kuajiriwa, waanzisha saluni zao
- Waliosajiliwa waongezeka kutoka 5,000 hadi zaidi ya 10,000
- Kampeni sasa kuhamia mikoani
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BAADHI ya wasusi walioshiriki programu ya Loyalty ya kampuni ya Darling Hair wamefanikiwa kuongeza mitaji na wengine kutoka kuwa waajiriwa hadi kumiliki saluni zao.
Mafanikio hayo yameelezwa wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka miwili ya programu hiyo iliyofanyika Sinza, Dar es Salaam, ikiwakutanisha wasusi kutoka Tabata, Mbezi, Kimara na maeneo ya jirani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Salma Hamadi kutoka Tabata, alisema zawadi zinazopatikana kupitia programu hiyo zimekuwa nyenzo ya kuwawezesha wasusi kukuza biashara zao.
“Programu hii sasa ina miaka miwili na tayari tumeona makubwa. Baadhi yetu tumeongeza mitaji na wengine walioanza kama wasusi wa kuajiriwa sasa wana saluni zao baada ya kujishindia vifaa mbalimbali,” alisema Salma.
Aliipongeza Darling Hair kwa kuwajumuisha wasusi katika programu hiyo na kuwakutanisha kila mwaka kwa ajili ya kutambua kazi zao na kuwazawadia.
Doreen Didas wa Mbezi Mwisho aliwataka wasusi kutumia fursa hiyo kwa kukusanya lebo zinazowaongezea pointi ili kupata nafasi ya kushinda zawadi zitakazosaidia kukuza biashara zao.
“Unaweza kuwa msusi mdogo, lakini Darling Hair wakakusaidia kukua polepole kupitia programu hii ya Loyalty,” alisema.
Naye Shantel Mushi wa Tabata Mawenzi alisema programu hiyo imefungua fursa kwa wasusi kujiongezea vifaa na mitaji, akiwahimiza ambao hawajajiunga kufanya hivyo.

“Natamani wasusi wote waijue programu hii. Ambao hamjajiunga mmechelewa, lakini bado mna nafasi ya kujiunga na kunufaika kama sisi,” alisema Shantel.
Angel Ngita wa Tabata alisema ameamua kuendelea kukusanya pointi badala ya kuchukua zawadi aliyokuwa ameshinda, akilenga kupata zawadi yenye thamani kubwa zaidi itakayomsaidia kuendeleza biashara.
“Mimi leo nimeshinda, lakini sichukui zawadi. Naendelea kukusanya pointi ili nipate kitu kikubwa zaidi. Nimeingia kwenye programu hii nikiwa na malengo ya kujiendeleza,” alisema.
Christina Mbando, pia kutoka Tabata, alisema ukaribu wa kampuni hiyo na wasusi umewasaidia baadhi yao kupiga hatua katika shughuli zao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Darling Hair, Daniel Kisusange, alisema programu hiyo imepanuka kwa kasi katika kipindi cha miaka miwili.
Alisema mwaka wa kwanza walianza na wasusi 5,000, lakini idadi hiyo sasa imevuka 10,000.
“Lengo ni kuwainua wasusi wadogo ili wapate mitaji na hatimaye waweze kujiajiri wenyewe,” alisema Kisusange.
Alisema baada ya kufanyika Dar es Salaam, kampeni hiyo inatarajiwa kuhamia mikoani ili kuwafikia wasusi wengi zaidi nchini.
“Tunawaomba mjiandae, tunakuja huko. Kampeni hii ni ya nchi nzima na lengo ni kuendelea kuwafikia wasusi wengi zaidi,” alisema.
Kisusange alisema Loyalty ni programu ya kudumu ya kampuni hiyo, hivyo akawahimiza wasusi kuitumia kama fursa ya kukuza shughuli na mitaji yao


