Waishukuru Serikali kuwapelekea huduma ya matibabu ya moyo Z’bar

Na Mwandishi Maalum – Zanzibar

Wakazi wa Zanzibar wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea huduma ya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima inayotolewa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani humo.

Huduma hiyo inatolewa bila malipo katika kambi maalumu ya siku tano inayofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Visiwani Zanzibar wananchi waliofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo walisema kupatikana kwa huduma hiyo kumewarahisishia tofauti na ambavyo wangeifuata huduma hiyo Dar es Salaam.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) George Longopa akimfanyia mgonjwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) leo wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano  inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar.

Saada Simba mkazi wa Fuoni amesema baada ya kusikia wataalamu wa moyo watakuwepo katika Hospitali hiyo alifika kwa ajili ya kupima afya yake amefarijika kwani amepata huduma nzuri na kwa wepesi.

“Mimi ninatatizo la shinikizo la juu la damu (BP) baada ya kufanyiwa vipimo leo nimekutwa sina tatizo lolote zaidi ya hili nililokuwa nalo, nashukuru sana nimepewa ushauri na nimeongezewa dawa nyingine ya kutumia ambayo ninaenda kuichukuwa dirishani bila malipo yoyote yale”, amesema Saada.

Naye Juma Amoor mkazi wa alisema akiwa kazini mwaka 2019 alipata mshtuko wa moyo kwani mapigo yake yalikuwa yanadunda kwa kasi alifanyiwa uchunguzi na kuandikiwa dawa za kutumia lakini alifika hapo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na kujua tatizo ni nini.

“Nawashauri wananchi wenzangu tujenge tabia ya kupima afya zetu pindi tunaposikia wataalamu kama hawa wamefika katika maeneo yetu twendeni kupima. Baada ya kufika hapa leo nimepima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), mfumo wa umeme wa moyo (ECG), kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu, urefu na uzito bila malipo yoyote yale”, amesema Amoor.

Maafisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji na mwenzake wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar Salama Rashid wakitoa elimu ya jinsi ya kuandaa chakula bora kwa mwananchi aliyefika katika Hospitali hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya siku tano   inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya  Mnazi Mmoja  Zanzibar

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha utafiti na mafunzo cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo amesema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kusogeza huduma zake kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo na kuwapatia huduma ya upimaji na matibabu ya moyo.

Dkt. Pedro amesema kuwepo kwa huduma hiyo kumewasaidia wananchi kupata huduma ya ushauri wa lishe na matumizi sahihi ya dawa, vipimo na matibabu ya moyo kwa wakati tofauti na ambavyo wangesafiri na kuifuata huduma hiyo Dar es Salaam pia wanaokutwa na matatizo wanapewa rufaa ya kwenda kufanyiwa uchunguzi zaidi katika Taasisi hiyo.

Dkt. Pedro amesema, “Ninatoa wito kwa wananchi kufuata mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kupunguza matumizi makubwa ya sukari, chumvi na vyakula vyenye mafuta, kupunguza unywaji wa pombe na kuacha kutumia bidhaa aina ya tumbaku kwa kufanya hivyo wataepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo”,.

Daktari wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jackline Mathew akimfanyia mtoto kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) leo wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano  inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar.

Katika kutoa huduma ya kuwafuata wananchi mahali walipo Taasisi hiyo kwa mwaka 2022 ilifanya upimaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Geita, Mtwara na Lindi na kuwahudumia watu 3,935 kati ya hao 1,391 walikutwa ma magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la damu, kutanuka kwa misuli ya moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, matundu ya moyo hasa kwa watoto na valvu za moyo zilizoharibika. Wagonjwa 335 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.