Waliojiua wakitaka kukutana na Yesu wafukuliwa

Polisi nchini Kenya walisema Ijumaa kwamba wamefukua miili ya watu watatu, inayodhaniwa kuwa ya wafuasi wa dhehebu la kidini wanaoaminika walijiua kwa njaa, mashariki mwa nchi hiyo wakati wakati polisi imepanua uchunguzi wake.

“Mchakato wa kufukua miili bado unaendelea na mpaka sasa maiti mitatu zimepatikana” alisema Charles Kamau, mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai katika wilaya ya Malindi, ikiashiria maiti hizo hazijatambuliwa na chanzo cha vifo vyao hakijajulikana.

Makenzie Nthenge, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Good News International, alijisalimisha kwa polisi na kufunguliwa mashtaka mwezi uliopita, kulingana na vyombo vya habari vya Kenya, kufuatia vifo vya watoto wawili waliokufa kwa njaa wakiwa mikononi mwa wazazi wao.

Baadaye kiongozi huyo aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 100,000 za Kenya.

Polisi waliripoti kukamatwa kwake Jumamosi iliyopita baada ya kugundua miili ya wafuasi wanne ambao inasemekana aliwaambia wasile ili “wakutane na Yesu”

Wafuasi wengine 11 wa kanisa hilo mmoja wao mdogo zaidi mwenye umri wa miaka 17 walipelekwa hospitali, watatu kati yao wakiwa mahututi, baada ya kuokolewa wiki moja iliyopita pale maiti za mwanzo zilipogunduliwa kwenye msitu uliopo nje ya mji wa Malindi ulioko pwani ya mashariki.

Kamau alisema miili iliyopatikana hivi karibuni pia ilikuwa katika msitu wa Shakahola kufuatia uchunguzi wa kina katika eneo linalodhaniwa kuwa na kaburi la halaiki.

Polisi walivamia msitu huo baada ya kupata taarifa za vifo vya “wananchi wajinga wanaokufa kwa njaa kwa kisingizio cha kukutana na Yesu baada ya kuchotwa akili” na Nthenge.