Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Katavi

Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumteka mtoto mdogo wa (9) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Msingi Mizengo Pinda katika Manispaa ya Mpanda na kisha kumfungia ndani na kutaka walipwe milioni 50 ili wamwachie mtoto huyo .

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani amewataja watuhumiwa hao walikamatwa kuhusika na tukio hili kuwa ni Joseph John (24), Yusuph Sadick (27) wakazi wa Mtaa wa Milupwa, Abrahamu Kassim (28), Mkazi wa Mtaa wa Misunkumilo Manispaa ya Mpanda na Samwel Nzobe (41), mkazi wa Mtaa wa Kotasi Manispaa ya Mpanda .

Amesema watuhumiwa hao wote wanne wamekamatwa kufuatia msako mkali ulifanywa na Jeshi la Polisi usiku na mchana na kufanikiwa kumpata.

Kaimu Kamanda wa Polisi Ngonyani amebainisha kuwa tukio hilo la kikatili lilitokea Juni 13, majira ya saa 8, mchana katika Manispaa ya Mpanda wakati mtoto huyo alipokuwa akitoka shule ya Mizengo Pinda alikokuwa amekwenda kufanya usafi shule.

Ameeleza kuwa wakati akiwa njia maeneo ya jirani na Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda akielekea nyumbani ndipo watuhumiwa hao wanne walipomteka mtoto huyo na kumpeleka kusiko julikana na kumtishia kumuua lasivyo walipwe na mzazi wake kiasi cha shilingi milioni 50 ndipo waweze kumwachia akiwa hai .

Baada ya taarifa Jeshi la Polisi lilianza mara moja kufanya msako mkali wa kuwasaka wahusika wa tukio hilo msako ambao ulifanyika usiku na mchana katika maeneo yote ya Mkoa wa Katavi.

Ngonyani amesema ndipo Juni 14,Jeshi la Polisi walifanikiwa kumpata mtoto huyo akiwa salama huko katika maeneo ya Mtaa wa Milupwa Manispaa ya Mpanda akiwa amefichwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa Joseph John.

Amesema watuhumiwa wote wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hili na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili .

Please follow and like us:
Pin Share