Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Rufiji

SERIKALI inaendelea kurekebisha miundombinu ya elimu ambayo imeathiriwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha ,na kuagiza wanafunzi wote walio kwenye maeneo ambayo yameathiriwa na mafuriko kote nchini wahakikishe wanaendelea na shule .

Aidha wazazi na walezi wa watoto hao pamoja na wale wenye watoto wenye mahitaji maalum wasiwaache nyumbani ,bali wawasiliane na viongozi ama ngazi ya elimu vijiji na kata ili kushirikiana kuwapeleka watoto shule.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknoloji Prof. Adolf Mkenda alitoa wito huo ,wakati alipotembelea miundombinu ya elimu kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko, Muhoro wilayani Rufiji, mkoani Pwani.

Hata hivyo Mkenda aliwaasa ,walimu kuwapokea wanafunzi ambao shule zao zimekumbwa na mafuriko ili waendelee na masomo wakati serikali ikiwa inaendelea na juhudi za kuhakikisha miundo mbinu ya elimu inarejea kama kawaida.

“Serikali inajitahidi kuweka miundombinu kwenye mahitaji taarifa zipelekwe kwa viongozi wanaohusika ili watoto wetu waendelee kusoma”alifafanua Mkenda.

Nae Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakar Kunenge, alieleza kwamba Serikali itahahakikisha wananchi walioathiriwa na mafuriko wanabaki salama.

“Kama Serikali tutahahakikisha wananchi wanabaki salama, katika maeneo salama ikiwa ni kuwahamisha katika maeneo ambayo yanaathiriwa na mvua na maafa ya mafuriko kila mwaka,mara kwa mara.”alieleza Kunenge.

Kunenge alieleza, watafanya linalowezekana kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

“Lazima niwe mkweli hatuwezi kila mwaka tukaja katika hali hii,ni wajibu wa Serikali kushughulikia maisha ya wananchi na kuhakikisha wanakuwa salama.” anabainisha Kunenge.

 

 

 

 

 

 

 

Please follow and like us:
Pin Share