Wakubaliana Kulinda Taaluma Yao kwa Wivu Mkubwa
Wataka Habari Ziwe na Tija kwa Watanzania
Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Wadau wa Vyombo vya Habari nchini wamekutana na kujadiliana kuhusu mustakabali mpya wa sekta ya habari kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi za habari sambamba na kuzalisha madhui yenye tija kwa Taifa.
Wakizungumza leo Aprili 29, 2026 jijini Arusha katika mjadala kuhusu Vyombo vya Habari, Ubunifu na Teknolojia: Nini Kifanyike kwa Ajili ya Uendelevu wa Vyombo vya Habari Nchini, ambapo kesho ni kilele cha Maadhimisho hayo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bw. Isaack Mruma amesema kuwa Tanzania sio kisiwa kwenye masuala ya usimamizi wa Vyombo vya Habari na kuwa Vyombo vya Habari hupewa haki ya kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Katibu Mtendaji wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Bi. Jacqueline Lawrence amesema kuwa Vyombo vya Habari nchini vilianza mwaka 1994, hivyo kuendeleza uwepo wa wadau katika Bodi zinazohusika na masuala ya habari ni muhimu ili kuleta uelewa na ushirikishwaji kati ya Serikali na wadau.
Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile amesema kuwa taaluma ya habari ni nyeti, ikiwa itatumiwa na watu wasio na sifa za kitaaluma inaweza kuleta madhara kwa jamii, hivyo imepongeza jitihada za Serikali za kuhakikisha taaluma hiyo inakuwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ambayo inasimamiwa na wajumbe ambao ni wanataaluma.
“Hakuna atakayekuja kulinda taaluma yetu, hii ni taaluma nyeti, iwapo itatumika vibaya inaweza kuleta madhara, pia ni lazima kuwe na kiwango cha elimu ili mtu aweze kuwa mwandishi wa habari,” amesema Balile.
Ameendelea kusema kuwa, kupitia Maadhimisho hayo , Vyombo vya Habari vinatakiwa kujadili kuhusu vyanzo vipya vya mapato yatakayoweza kuendesha vyombo vyao akitolea mfano Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kupitia kifungu cha pili na tatu ambavyo vinazungumzia vyanzo vya mapato ikiwemo Mfuko wa Baraza la Habari huku akiomba Serikali kufikiria kuwezesha Mfuko huo kwa kutoa fedha zitakazotumika kuvikopesha Vyombo vya Habari ili viweze kujiendesha kwa ufanisi.
Aidha, wadau hao wamezungumzia kuhusu haja ya Vyombo vya Habari kufanya maboresho kwa kuwa habari ni huduma na sio biashara.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben amesema kuwa Vyombo vya Habari vinaweza kuiomba Serikali kufanyia kazi sheria za uwekezaji katika huduma ya habari na utangazaji ili kuipunguzia kodi katika vifaa vyenye thamani kubwa kwa lengo la kuvisaidia Vyombo hivyo kujiendesha kwa ufanisi.
Pia, ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuzingatia weledi wa taaluma yao na kuwa wabunifu wanaporipoti habari.
“Waandishi wa habari tuandike habari zetu kwa kina, tuwe na vyanzo vya habari vya kutosha katika habari na makala zetu. Wanahabari tuhakikishe hatupitwi na wakati na mamlaka zinazosimamia sekta hii zifahamu namna vyombo hivi vinavyojiendesha ili kuleta tija kwa wanahabari wenyewe na vyombo hivi viandike habari kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Reuben.
Ameongeza kuwa changamoto zilizopo katika sekta hiyo zijadiliwe na kupatiwa ufumbuzi, badala ya kudhani Serikali au watu fulani wanaweza kuwa na changamoto.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Ithibadi ya Waandishi wa Habari (JAB), Dkt. Egebert Mkoko amesema kuwa mwaka 2016 wadau walishiriki kikamilifu katika kuunda Sheria ya Huduma za Habari na walikubaliana mambo ya msingi ikiwemo uandishi wa habari kuwa taaluma.
“Mahali popote duniani lazima kuwe na vigezo ikiwemo cha elimu na Bodi ya kusimamia taaluma na kutoa leseni, sisi Tanzania tunafanya hayo kupitia JAB.





