Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe

RAIS wa Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu ambazo kitaifa zinafanyika mkoani Njombe.

Hayo yamesemwa leo Aprili 29,2026, na Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema maandalizi yamekamilika.

Mtaka amesema mkoa umejiandaa kwa ugeni huo na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika Kiwanja cha kilichopo ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe.

Amesema mkoa umejipanga vizuri kwenye eneo la ulinzi na usalama, hivyo kuwataka washiriki wasiwe na wasiwasi.

“Mei mosi mwaka huu inafanyika hapa kwetu Njombe na mgeni rasmi ni Rais Samia nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kusherehekea na kiongozi wetu na wafanyakazi,” amesema.

Mtaka ametaja kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya Mei Mosi ni kazi zenye staha ni nguzo imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, hivyo ni muhimu wananchi kujitokeza ili kumsikiliza kiongozi wao.

Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema wamejiandaa vizuri kumpokea Rais Samia na kwamba matumaini yao ni kuona akizungumzia maslahi ya wafanyakazi.

Amesema TUCTA ina wajibu wa kuwahimiza wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji, hali ambayo itaongeza mapato na kukuza uchumi.

“Najua wafanyakazi wanataka kujua mwaka huu mshahara utaongezwa, hilo napenda kuwaomba tumsubiri Rais siku ya Mei Mosi,”