Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme katika vitongoji 105 mkoani Mbeya wenye thamani ya shilingi bilioni 10.9 unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO).

Wakikagua maendeleo ya mradi huo, Aprili 29, 2026 Mkoani Mbeya, wajumbe wa bodi hiyo, wakiongozwa na muwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Bw. Florian Haule, wamesema wameridhika na kasi ya utekelezaji na kumpongeza mkandarasi kwa kufanikisha hatua kubwa ya mradi, ambao hadi sasa umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Abdallah Mitenda, amesema kuwa Kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha mradi unakamilika mwishoni mwa Mei 2026, hivyo kukamilika ndani ya mwaka mmoja badala ya miaka miwili kama iliyopangwa kwenye mkataba.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka ETDCO, Mhandisi Ajuaye Jeggo, amesema kuwa kupitia mradi huo wanatarajia kuunganisha wateja takribani 3,465, huku akitoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayofikiwa na mradi huo kwa kufanya maandalizi ya ndani ya nyumba ( wiring) ili waweze kuunganishiwa umeme mara moja pindi huduma itakapoanza kwa gharama ya shilingi 27,000

Nao, wananchi Mkoa wa Mbeya, wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini kwa kuwaletea mradi huo kwani utasiadia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yao.

Mradi huo unaotekelezwa na ETDCO unahusisha ujenzi wa laini ya umeme ya msongo wa kati yenye urefu wa takribani kilomita 1.5, laini ya msongo mdogo yenye urefu wa kilomita 210 pamoja na uwekaji wa mashine umba (Transformer) 105.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakikagua mradi wa kuunganisha umeme katika vitongoji 105 mkoani Mbeya wenye thamaniĀ  ya shilingi bilioni 10.9 unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO).