Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Namtumbo 

Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WEF)  umetoa  mkopo zaidi ya shilingi milioni 287  tangu mwaka 2015 hadi 2024 Kwa wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na , Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya wakati anazungumza  kwenye maadhimisho ya Siku ya mwanamke Duniani kiwilaya kwenye ukumbi wa  shule ya Sekondari Nasuli.

Malenya amelitaja kundi la wanawake kuwa ni nguvu kazi kubwa kulingana na wingi wao.

 Hata hivyo amesema wanawake wamekuwa wakinyanyashwa, kukandamizwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili.

“Nawaasa wanangu wa jinsia ya kike endeleeni kuchukuwa tahadhari hakikisheni wale wanaume wanaowamendea wasiwapate, tunataka nyinyi muwe sehemu ya ushuhuda wa awamu ya Sita kwa maendeleo ya mwanamke “. amesema Malenya.

Ametahadharisha kuwa wilaya ya Namtumbo imeathiriwa Kwa janga la UKIMWI ambapo takwimu zinaonesha kuwa wanawake walioathirika idadi yao ni kubwa kuliko wanaume.

Ametoa rai kwa Taasisi  za kifedha  kuendelea kuboresha huduma rafiki katika kuwafikia wanawake wengi na kuwapa mikopo yenye riba nafuu 

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Namtumbo Peresi Kamugisha amesema Serikali imewekeza katika afya Ili kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua na kwamba serikali imeimarisha miundo mbinu ya shule maalumu za watoto wa kike katika wilaya ya Namtumbo.

Kwa upande wake Afisa USTAWI  wa Jamii wilaya ya Namtumbo Frida kayombo amesema ukatili wa kijinsi ni matumizi mabaya ya nguvu  na huleta madhara kimwili, kiakili.

Naye Mhamasishaji wa Damu Salama Wilaya ya Namtumbo Godfrey Mwaulesi  amewaomba wakinamama  kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wanaosumbuliwa na tatizo la damu kama wakinamama wanaojifungua na kupoteza damu nyingi na watu wanaopata ajali.

 Mkuu  wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya akimkabidhi taulo za kike mwanafunzi wa sekondari ya Nasuli ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku mwanamke Duniani