Takriban watu 35 wamefariki baada ya kutumbukia kwenye kisima walipokuwa wakisali katika hekalu moja katika jimbo la kati la India la Madhya Pradesh.

Wengine 14 wameokolewa na mtu mmoja bado hajapatikana katika ajali hiyo iliyotokea katika mji wa Indore.

Polisi wanasema waathiriwa walikuwa wamesimama kwenye slab ya zege juu ya kisima kilipoporomoka chini ya uzani wao.

Waziri Mkuu Narendra Modi alisema ‘aliumizwa sana na ajali hiyo.

Kisa hicho kilitokea siku ya Alhamisi wakati wa hafla ya maombi iliyoandaliwa katika hekalu la Beleshwar Mahadev Jhulelal kwenye hafla ya sherehe ya Kihindu ya Ram Navami.

Umati mkubwa wa waumini walikuwa wamesimama kwenye slab ya zege iliyofunika kisima ambacho kiliporomoka kwa uzito wao, na kuwatumbukiza watu wengi kwenye kisima chenye kina cha futi 40 (12m).

Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba hekalu hilo lilijengwa baada ya kisima hicho kufunikwa takriban miongo minne iliyopita.

Afisa mkuu Illayaraja T aliambia kituo cha habari cha ANI kuwa watu 18 walilazwa katika hospitali hiyo baada ya kuokolewa na watu wawili wameruhusiwa kufikia sasa.

Aliongeza kuwa msako bado unaendelea ili kumpata mtu aliyetoweka.

Timu ya wafanyakazi 75, ikiwa ni pamoja na wale wa serikali na vikosi vya kitaifa vya kukabiliana na maafa wanashiriki katika juhudi za uokoaji.

Waziri Mkuu Shivraj Singh Chouhan ametangaza fidia ya rupia 500,000 ($6000; £4900) kwa jamaa wa marehemu na rupia 50,000 kwa waliojeruhiwa.

By Jamhuri