Na Mary Gwera, JamhuriMedia, Mahakama

Mahakama ya Tanzania kupitia Kitengo cha Maboresho (JDU) imeandaa Mafunzo ya kujenga uelewa kwa Watumishi wake kuhusu matumizi ya Mfumo mpya wa Serikali wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao unaojulikana kama (NeST).

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama leo tarehe 15 Agosti, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Mahakama cha Masuala ya Mirathi na Ndoa Temeke-Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Challe amesema Mafunzo hayo yatasaidia kutekeleza na kusimamia michakato ya ununuzi ya Taasisi, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuleta uwazi.

Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Challe akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Mahakama kuhusu Mfumo Mpya wa Serikali wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao unaojulikana kama (NeST), Mafunzo hayo yamefunguliwa leo tarehe 15 Agosti, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Mahakama cha Masuala ya Mirathi na Ndoa Temeke-Dar es Salaam.

“Ninawaomba washiriki kufuatilia mafunzo haya kwa kina kwa manufaa ya Mahakama, Wazabuni, Wananchi na Taifa kwa ujumla hatimaye Watanzania kupata thamani ya fedha zao za kodi na vilevile kuondokana na hoja za ukaguzi zisizo na msingi,” amesema Bw. Challe.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa, Mafunzo hayo ya siku tano (5) yanatolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Mamlaka ambayo ndiyo iliyobuni Mfumo huo na ndio wenye jukumu la kutoa mafunzo na kusimamia utekelezaji wake.

“Mnatakiwa kuwa na umakini mkubwa sana kwani uelewa na utekelezaji wa mfumo huu ni matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuwa na matumizi mazuri na sahihi ya fedha za umma katika ununuzi wa vifaa na huduma na hatimaye kuwaletea Watanzania maendeleo yaliyokusudiwa,” amesisitiza Bw. Challe.

Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Challe akiendelea kuzungumza na Washiriki wa Mafunzo ya Mfumo Mpya wa Serikali wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao unaojulikana kama (NeST). Pamoja naye ni Wawezeshaji wa Mafunzo kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kushoto ni Bw. Furael Lema na kulia ni Bw. Joseph Kiphizi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Mahakama itaanza matumizi rasmi Mfumo wa ‘NeST’ Oktoba Mosi mwaka huu.

Mafunzo hayo yamehusisha jumla ya washiriki 51 kutoka Idara na Vitengo mbalimbali vya Mahakama. Na katika mafunzo hayo washiriki watapitishwa katika maeneo mbalimbali ya Mfumo ili waweze kuwa na uelewa wa kutosha kabla ya kuanza matumizi rasmi.

Washiriki wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ya ‘NeST’ iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Challe (hayupo katika picha) aliyefungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

By Jamhuri