Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete, amefungua Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania, akisisitiza kuwa utumishi wa umma una nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu isemayo, “Nafasi ya Utumishi wa Umma katika Kufanikisha Malengo ya Dira za Taifa 2050”, likiwa limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa na namna ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Ridhiwani amesema kuwa utumishi wa umma ndiyo nguzo imara ya utekelezaji wa sera, mipango na mikakati ya maendeleo, hivyo ni muhimu kuhakikisha watumishi wanajengewa uwezo na mazingira bora ya kazi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa 2050 kunategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa utumishi wa umma wenye weledi, uwajibikaji na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayoendelea duniani.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu Chuo cha Utumishi wa Umma Ernest Mabonesho amesema, kongamano hilo limejadili dhana mbalimbali zinazolenga kuangazia nafasi ya utumishi wa umma katika kuhimili na kuongoza mabadiliko, hususan katika eneo la mabadiliko ya kidijitali yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza tija katika taasisi za umma.

Washiriki wa kongamano wameeleza kuwa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utumishi wa umma yatachangia kuongeza uwazi, uwajibikaji na kasi ya utoaji huduma, sambamba na kusaidia serikali kufikia malengo yake ya maendeleo ya muda mrefu.

Kongamano hilo linatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa chachu ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa Tanzania kuelekea mwaka 2050.