Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde amebainisha kwamba Serikali kupitia Tume ya Madini imefuta jumla ya maombi ya leseni 227 ambayo yamekosa vigezo vya kuendelea kufanyiwa kazi.

Ameyasema hayo leo tarehe 24 Aprili, 2024 Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka kipaumbele katika kuendeleza sekta ya madini nchini. Ndugu zangu nataka niwaambie kwamba sisi Wizara ya Madini hatupo tayari kufifisha juhudi hizi njema za kiongozi wetu.”

“Na ndiyo maana mwezi uliopita tulitangaza kufuta jumla ya maombi na leseni 2,648. Wengi walidhani sisi tunafanya utani, nataka niwaambie Serikali hatupo tayari kuona watu wachache wanashikilia maeneo pasipo kuyaendeleza kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123.” Alieleza Mhe. Mavunde.

Pia, Mhe. Mavunde alibainisha kwamba maombi hayo 227 yamefutwa kutokana na sababu ya kutolipiwa ada stahiki za maombi kwa mujibu wa Sheria pamoja na kukosa nyaraka zinazotakiwa kuambatishwa na maombi hayo.

Aidha,Mhe. Mavunde alieleza kwamba uchambuzi uliofanywa na Tume ya Madini umebaini kuwa kuna watumiaji wa mfumo wa uwasilishaji maombi kwa njia ya mtandao wapatao 34 wanatumia mfumo vibaya kwa kuwasilisha maombi bila kulipa Ada stahiki.

Vilevile, Mhe. Mavunde alisisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Nchi yetu, na hivyo wale wote ambao hawapo tayari kufuata Sheria na taratibu za madini zilizopo hatafumbiwa macho.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde alieleza kwamba tangu alipotangaza kufuta leseni 2,648 mnamo tarehe 22 Machi, 2024 kumekuwepo na umakini mkubwa wa uwasilishaji wa maombi na kufanyika kwa malipo kwa mujibu wa sheria ambapo jumla ya mapato ya shilingi 2,430,647,335.99 yamekusanywa na Tume ya Madini, fedha hizo zimetokana na waombaji na wamiliki wengi wa leseni kuzingatia na kufuata taratibu za kulipia leseni na maombi yao kwa mujibu wa Sheria.

Akihitimisha taarifa yake, Mhe. Mavunde aliielekeza Tume ya Madini kuendelea na uchambuzi wa leseni na maombi ili kuendelea kubaini maombi na leseni ambayo hayakidhi vigezo vya kisheria kwa ajili ya kuendelea kufuta kupisha waombaji wengine wenye uhitaji wa kuendeleza maeneo hayo.