Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Kutokana na mabadiliko ya kidigitali kubadilisha mifumo kwa kiasi kikubwa katika jamii na pia kuwa na uwezo wa kuendelea kuleta mabadiliko mengine zaidi, wiki ya Asasi za Kiraia mwaka huu inayotarajiwa kuanza kesho jijini Arusha imelenga kukutana na Serikali, wananchi, wanazuoni pamoja na sekta binafsi kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya Taifa kiteknolojia.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo Oktoba 22, 2023 jijini hapa Mkurugenzi Mkazi wa CBM ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya wiki ya AZAKI, Nesia Mahenge amesema majadilianao hayo ni fursa ya kipekee ya kuchangamana na wadau wa maendeleo kwani wamelenga kuangalia jamii ilipotoka, ilipo hivi sasa na inakwenda wapi katika nyanja ya teknolojia ili kuelewa mabadiliko yaliyopo, kukabiliana na changamoto pamoja na kutumia fursa zinazotolewa.

“Kauli mbiu ya wiki ya AZAKI mwaka huu wa 2023 ni Teknolojia na Jamii, ambapo suala kubwa ambalo tutalizungumzia ni kujitathmini ni kwa kiasi gani tumeweza kutumia teknolojia katika miradi na kazi zetu, ikiwa ni pamoja na kuangalia ni maeneo gani ambayo tumejifunza na ni maeneo gani yana changamoto” amesema Mahenge.

Amesema lengo kuu la wiki ya AZAKI 2023 limebaki kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi, serikali na wananchi ambapo mijadala itakayojadiliwa imejikita zaidi katika ujumuishwaji wa teknolojia kwenye kazi za AZAKI, kuziwezesha na kuzipa nguvu jamii zilizotengwa, utetezi ushirikiano pamoja uchechemuzi wa kidigitali.

Mijadala mingine ni matumizi ya takwimu kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika jamii ikiwemo ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi, teknolojia na maadili, ubunifu wa teknolojia kwa maendeleo endelevu pamoja na kujadili ni kwa kiasi gani wameweza kufanikisha na ni katika maeneo gani wanahitaji kuboresha utendaji kazi wao.

“Aidha tutajadili mchango wa teknolojia katika kuboresha elimu, teknolijia katika utetezi wa jamii, teknolijia katika ushirikiano na kuboresha uwazi, teknolojia kwenye ujasiriamali na maendeleo endelevu, teknolojia katika kuimarisha usalama mtandaoni na hapa tutajikita kwenye changamoto za usalama wa mtandaoni zinazokabili AZAKI nchini na hatua za kulinda takwimu au data za siri kwa mawasiliano salama” amesema Mahenge.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dr. Anna Henga amesema mijadala hiyo pia itajikita katika masuala ya kimaadili katika kupokea matumizi ya maarifa bandia (Artificial Intelectual) ili kuhakikisha kuwa maarifa hayo yanalenga kukabiliana na changamoto za kijamii na kuleta manufaa kwa jamii nchini Tanzania.

Naye Mwakilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Deogratius Temba amesema katika kuhakikisha kauli mbiu ya mwaka huu ya Teknolojia na Jamii inakuwa jumuishi kwa jamii yote, watahakikisha makundi yaishio pembezoni hususani wanawake nao wanafikiwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Wiki ya AZAKI 2023 Nesia Mahenge akizungumza na waandishi wa habari.

By Jamhuri