Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii imewasilisha maombi ya kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi bilioni 359.98 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Maombi hayo yametolewa leo Mei 19, 2025 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Pindi Chana, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha ujao.

Kwa mujibu wa Waziri Chana, kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 254.23 zitatumika kwa Matumizi ya Kawaida huku Shilingi bilioni 105.74 zikitengwa kwa Miradi ya Maendeleo.
Akiendelea kufafanua, Waziri alisema kuwa katika Matumizi ya Kawaida, Shilingi bilioni 130.70 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi bilioni 123.52 kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, alisema Shilingi blioni 32.48 ni fedha za ndani, huku Shilingi bilioni 73.27 zikiwa ni fedha za nje kutoka kwa wahisani na washirika wa maendeleo.
Waziri alibainisha kuwa matumizi hayo yanakusudiwa kuimarisha sekta za uhifadhi, utalii, misitu, nyuki na malikale pamoja na kuongeza mapato kupitia shughuli za kiuchumi zinazotegemea rasilimali hizo.

Miongoni mwa vipaumbele vya wizara hiyo ni kutangaza utalii kimataifa kupitia mashindano ya michezo, mashirika ya ndege, matamasha na mitandao ya kimataifa sambamba na kuendeleza maeneo ya utalii wa fukwe, meli, michezo na tiba.
Wizara pia inalenga kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha matumizi ya teknolojia kisasa katika usimamizi wa rasilimali na ulinzi wa wanyamapori, misitu na malikale.
Katika mafanikio ya miaka minne iliyopita, mapato yatokanayo na utalii wa kimataifa yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi bilioni 3.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 200.
Aidha, mapato kutoka utalii wa ndani yamepanda kutoka Shilingi bilioni 11.46 mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 209.8 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 353.1. Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 132.1 hadi kufikia zaidi ya milioni 2.

Amesema kuwa Serikali Kupitia wizara hiyo pia imekusanya maduhuli ya Shilingi bilioni 901.08 mwaka 2023/2024 kutoka Shilingi bilioni 397.42 mwaka 2020/2021 ambapo hadi Aprili 2025, Shilingi bilioni 912.9 zimekusanywa sawa na asilimia 94.2 ya lengo.
amesema Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa kwa kushinda tuzo saba za utalii zikiwemo za Africa’s Leading Destination 2024 na World’s Leading Safari Destination 2024, huku Hifadhi ya Serengeti ikitambuliwa kwa miaka sita mfululizo kuwa bora duniani.
