Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

WIZARA ya Ujenzi imeandaa hafla ya kuelezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita kwa kipindi cha miaka mitatu katika sekta ya Ujenzi huku ikijinasibu kukamilisha miradi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wenye jumla ya kilometa 1, 198.50 .

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, tangu Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwezi Machi, 2021 jumla ya barabara 25 zimekamilika na 57 zenye urefu wa kilometa 3,794.11 zinaendelea na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Aprili 5,2024 Jijini hapa,Waziri Bashugwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imetenga miradi itakayotekelezwa na wazawa kwa lengo la kuwajengea uwezo makandarasi na Wahandisi Washauri elekezi wa ndani.

Amefafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 Wizara inatekeleza miradi 12 ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambayo imetengwa mahsusi kwa ajili ya Makandarasi Wazawa ikiwemo barabara ya Monduli – Engaruka – Ngareshi – Enguiki (km 11); Kamsamba – Mlowo (km 147); Changombe – Patamela – Makongolosi (km 30); na Puge – Ziba (km 11).

Bashungwa amesema,”Katika kipindi cha miaka mitatu Sekta ya Ujenzi imefanikisha ujenzi wa madaraja makubwa 8 yakiwemo Daraja la Wami mkoani Pwani, Daraja la Tanzanite mkoani Dar es Salaam, Daraja la Gerezani mkoani Dar es Salam, Daraja la Mpwapwa mkoani Dodoma, Daraja la Kiegeya mkoani Morogoro, Daraja la Ruhuhu mkoani Ruvuma, Daraja la Kitengule mkoani Kagera na Daraja la Msingi mkoani Singida,”amesema

Pamoja na mafanikio hayo, pia ameeleza kuwa kuna madaraja matano yapo katika hatua mbalimbali za Utekelezaji ikiwemo Daraja la J.P Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza ambao umefikia 85%, Daraja la Pangani mkoani Tanga umefikia 23%, Daraja la Mbambe mkoani Pwani umefikia 15% na Daraja la Mpiji Chini mkoani Dar es Salaam.

“Kuhusu utekelezaji wa Viwanja vya Ndege, Sekta ya Ujenzi imekamilisha Viwanja vya Ndege 5 vikiwemo Kiwanja Cha Ndege cha Geita, Mwanza, Mtwara, Songwe na Songea,miradi mingine ya Viwanja vya Ndege ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Kile cha Kimataifa cha Msalato, Iringa, Kigoma , Moshi, Musoma, Sumbawanga, Shinyanga na Tabora, “amefafanua

By Jamhuri