Tuko ukingoni kabisa mwa mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka ujao, mwaka ambao utakuwa na matukio mengi ya kisiasa na maendeleo, nimejitolea kuwa mnajimu kwa sasa hasa kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini na nje ya nchi yetu hususani Afrika Mashariki na Kati.

Kuna maneno ambayo yanazungumzwa na watu wa ndani ya nchi na nje ambayo yanasemwa juu ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, wanapongeza sana lakini pia wapo ambao wanadai kuwa mbinu hiyo ilikuwa yao, wapo wanaopinga pia kasi ambayo inatumika katika kulitumikia Taifa, nadhani nafasi hiyo wangelipata wao basi sasa hivi yangekuwa yamefanyika mengi zaidi ya yaliyofanywa.

Kwangu mimi, lakini sina hakika sana na ninachoweza kusema ni kwamba matumizi ya demokrasia yamezidi na yanaweza kuleta athari kama hatutaweza kuyadhibiti kwa kuyapa mipaka ambayo itakuwa mbali kidogo na siasa, kujadili mambo ya kitaifa na kutoa suluhisho la jambo la msingi.

Kwa malezi yetu kama Watanzania tumekuwa tukiitumia demokrasia kama sehemu ya kujenga hoja na kujipatia umaarufu, wengi wetu imekuwa ni desturi kutumia mgongo wa demokrasia kuweza kujenga hoja zisizotekelezeka na hoja za ushindi wa jambo ambalo halijafanyika na halitaweza kufanyika, ni kitengo maalumu cha watu maalumu kuendesha maisha kwa kisingizio cha siasa.

Ni rahisi sana kuona upungufu wa mtu mwingine katika kazi lakini pia ni rahisi sana kutoweza kufanya ambacho unakitolea mawazo kama mshauri, hii ni taaluma mojawapo katika ya ngazi za kiutumishi. Kuna suala la kufikirika na suala la utendaji, wapo wanaoweza kutenda kwa mawazo lakini kivitendo ni rahisi sana kwa ngamia kupita katika tundu la sindano.

Hivi sasa wapo wanaoponda utaratibu wa viongozi wa Awamu ya Tano akiwamo kiongozi wao mkuu na hatua ambazo anazichukua, wakati wapingaji wakifanya hivyo wanazuoni wa kada mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wanapongeza hatua ambazo zinafanyika, wapo hata waliofikia kuufananisha utawala huu na kujitoa muhanga kwa suala hilo.

Wana demokrasia hawa wanazungumza kama vile wao wangeweza kufanya zaidi ya kile ambacho mpaka sasa Serikali imekifanya, wanazungumza kana kwamba utaratibu unaotumika wa kuzima moto kwa kutumia moto ni makosa na Serikali  ilipaswa kutumia maji badala ya moto, lakini ukweli ni kwamba wangetumia staili ya maji kuzima moto, watu hao wangekuwa na wakati mwingi zaidi wa kulaumu badala ya kupongeza hatua iliyochukuliwa, haya ndiyo matatizo ya demokrasia inapokuwa kubwa kuliko ukweli wa mfumo wa siasa wenyewe.

Kwangu mimi demokrasia ni tatizo la mfumo wa uvivu katika utendaji, naliona kama ombwe la kuficha watu ambao hawako tayari kufanya kazi, lakini wapo tayari kutoa ushauri wa kupinga ili uwepo wao uweze kudhihirika katika jamii ya watendaji, ni kundi la watu wanaojua kujenga hoja za kubomoa tu na siyo kujenga hoja za kusifia jambo jema ambalo limetokea.

Sasa hivi tupo katika mbiombio za kiutawala kuleta maendeleo ya nchi yetu, ni mbio za watawala na watawaliwa kupokezana vijiti na kufanya kazi kama mchwa, lakini pia wapo ambao wanalijua hilo na wao kazi yao kubwa ni kupinga chochote ambacho kinafanyika katika kuonesha jitihada zinazofanyika hadi sasa kwa maana ya kujiletea maendeleo.

Utaratibu wanaotumia ni kupinga kwa hoja, huku wakirejelea makosa ambayo yalifanywa na watu wengine, zipo hoja zenye mashiko na zipo hoja za kisiasa kuthibitisha kuwa wao ni wapinzani ama wao hawakutaka atende hivyo, zipo hoja za ubinafsi ambazo unaziona dhahiri kuwa zinatokana na wivu wa kimadaraka/

Lakini ukweli unabaki palepale kwamba linapokuja suala la kitaifa kwa manufaa na maendeleo ya taifa hatuna budi kuziweka tofauti zetu pembeni na kuacha kutumia fursa ya demokrasia kuvuruga jambo la msingi.

Tuna vita mbele ya kuwatambua maadui zetu katika kujiletea mabadiliko ambayo tulikuwa tunadai kwa muda mrefu, tunapotaka mabadiliko hatuna budi kukubali kubadilika ili tupate mabadiliko, tunapomgundua adui yetu  hatuna budi kuacha unafiki bali ni kumwambia kuwa wewe ni mwongo na unataka tusipate mabadiliko.

Ni vema tukaunga mkono jitihada ambazo zinafanyika na tukaweka pembeni tofauti zetu za kiitikadi na vyama ili tuweze kusonga mbele.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri