Siku kadhaa zilizopita, tumesikia baadhi ya miswada ya sheria ikiwa inafanyiwa kazi, kitu kizuri zaidi ni jinsi ambavyo sheria zilivyobainishwa na kuwa sheria nzuri kwa maana ya ukali wake kwa jamii ambayo ikikosea kufuata masharti itawajibika na adhabu hiyo.
  Kuna miswada mizuri ya sheria ambayo tunaisikia, baadhi inapitishwa baada ya kuboreshwa na mingine haipiti kutokana na sababu mbalimbali ambazo nyingine tunapaswa kujua tu kwamba zina maslahi binafsi na nyingine kutojua kwa watunga sheria umuhimu wake katika jamii yetu.


  Nchi yetu inapita katika wakati mgumu sana, tukiwa tunaandamwa na tatizo sugu la rushwa, dawa za kulevya ambazo sasa ni kama wanataka kuishika dola kwa kuwa mtandao wao ni mkubwa kiasi cha kushindwa kuwadhibiti, na hata kama ikitokea anayeweza kudhibitiwa ni dagaa mbele ya papa.
  Ukiacha mambo haya mawili, tuna tatizo la ujambazi na wizi uliokubuhu, hivi sasa imefika mahali hata askari anauawa ili kupata silaha za kuhalalisha kazi ya ujambazi mbele ya safari, tuna tatizo la ufisadi uliokubuhu pia ambao kutokana na uwezo wa mafisadi sasa wanatumia mbinu za kisheria zaidi kuweza kujilinda dhidi ya uhalifu huo. Hii ndiyo Tanzania ambayo naijua mimi.


  Japokuwa si siku za hivi karibuni tu pia kuna tatizo la kuwaua ndugu zetu maalbino kwa kisingizio cha kupata mali na kadhalika. Huu utaratibu unafanywa na kushawishiwa na watu wanaoitwa waganga wa jadi ambao wamejitahidi kuhalalisha kazi yao kuwa ni muhimu kwa jamii yetu.
 Haya yote yanafanyika ikiwa ni ndani ya mfumo wa Serikali ambayo inatakiwa kuwa makini na jambo lolote ambalo ni hatari kwa maisha ya Mtanzania mwenye nchi yake. Zamani haya mambo yalikuwa yakifanywa lakini sheria ilifuata mkondo na wengi wao walipotea katika Tanzania yenye kujali haki ya mtu na mali zake.


  Siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kuwateka ndugu zetu albino na kuwaua kwa maelezo kwamba viungo vyao ni chachu ya kujitajirisha, baadhi ya wauaji wamekamatwa na wako mbele ya vyombo vya sheria, lakini ukweli ni kwamba hawa wauaji mbali ya wao kuwa na mahitaji, kuna mtu anayewaelekeza kufanya ukatili huo.


  Kinachofanyika ni kumtafuta aliyekwishatenda kosa hilo lakini si yule anayesababisha madhara haya yatokee, huyu anayesababisha ndiye mbaya zaidi kwani anaweza kuwaagiza hata watu mia kwa siku wakalete viungo vya binadamu wenzetu. Nimeamua kuandika waraka huu kwa makusudi kuiuliza Serikali yetu ni mahali gani na sheria gani iliyoandikwa ya kukubali uganga wa kienyeji katika nchi yetu ya Tanzania?


  Na kama ipo, hiyo sheria ni wapi ambako waganga hawa wanadhibitiwa na chombo maalum ili kujua kama tiba zao zina athari kwa jamii yetu! Sitaki kusema moja kwa moja kwamba muswada wa sheria hii unaweza kushindwa kupitishwa kutokana na wengi wetu kuwa na imani na hawa waganga wa kienyeji, lakini napenda kutahadharisha kwamba madhara yake yanaweza kuwafikia hata wao iwapo tutashindwa kudhibiti hivi sasa kwa makini zaidi.


  Kuwa na imani za kishirikina ni kutokana na upumbavu, na upumbavu ni kipaji, ni  udogo wa ubongo wa kufikiria na pia ni ugonjwa unaohitaji tiba ikiambatana na ushauri nasaha zaidi, ili kuweza kumtoa mtu huyo katika imani aliyokuwa nayo.
  Uhuru huu walionao waganga wa kienyeji hapa nchini unasikitisha sana, waganga wamefikia mahali wanajitangaza hadharani mbele ya kadamnasi huku wakiweka mabango ya kutangaza biashara yao na yanaweza yakawa yanalipiwa ushuru japo sina hakika.


  Uhuru wa waganga wa kienyeji Tanzania umetufikisha hapa, na vyombo vya dola vipo lakini labda hatuna sheria ya kuwadhibiti, mimi naogopa hali hii ikiendelea tunazidi kuimarisha nguvu za giza nchini, hivi sasa tunaambiwa hata watoto wachanga ni dawa na bado tunashuhudia wanavyoibwa na kuuawa.
  Ombi langu ni kutaka iwepo sheria ya kuwamaliza hawa waganga wa kienyeji hapa nchini, kuwamaliza kwa maana ya kuwadhibiti na kuwafutilia mbali ili kuweza kupoteza hii dhana kwamba uganga ni kudhuru. Nchi zote zilizoendelea na zinazoendelea hawafikirii nguvu za giza katika maendeleo yao.


  Hili ni ombi tu kwa wenye mamlaka, bila kufanya hivyo tutaendelea kusikia vilio kila siku na bahati mbaya zaidi wanaoathirika ni watu wasio na hatia na wanaotudhuru ni wapumbavu ambao wanataka kuipeleka nchi kwa ujinga wao.

Wasalamu
Mzee  Zuzu
Kipatimo.

By Jamhuri