Huku ikiendelea na harakati za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Dar es Salaam Young Africans ‘Yanga’, yenye makao yake makuu mitaa ya Twiga na Jangwani, Jijini, inaendelea na mikakati ya kushinda mechi yake na Zesco, kutoka Zambia.

Mechi ya kwanza kati ya klabu hiyo na Wazambia hao inatarajiwa kuchezwa Jumamosi, jijini na kurudiana wiki moja baadaye, mjini Lusaka, Zambia.

Kumekuwapo na maneno kwamba kutokana na hali Klabu ya Yanga, inaweza kutumia usafiri wa reli ya Tazara, kama watatumia usafiri huo, itakuwa ni mara kwanza katika miaka ya hivi karibuni kutumia usafiri huo.

Klabu ya Yanga, maarufu kama ‘Wa Kimataifa’ wamekuwa wakishiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, katika mechi zao zote za ugenini pamoja na kambi nje ya nchi wamekuwa wakitumia usafiri wa ndege.

Akizungumza na JAMHURI juu ya hali taarifa hizo za timu kusafiri kwa kutumia treni, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema hayo ni maneno ya watu wasiyoitakia mema klabu yake.

Amesema Yanga ni klabu kubwa yenye wanachama ndani na nje ya nchi, klabu hiyo ina utamaduni wake na kamwe haiwezi kufanya kazi kwa maneno kutoka kwenye mitandao.

“Mechi yetu na Zesco haitakuwa rahisi… tunawaheshimu kama moja ya klabu kubwa nchini Zambia lakini kutokana na maandalizi ambayo benchi la ufundi linaendelea nayo, hatuna wasiwasi wowote,” amesema Mkwasa.

Mkwasa, ambaye amewahi kuwa kocha wa Yanga kabla ya kwenda kuifundisha Taifa Stars, amesema kabla ya mechi hiyo ya kimataifa, macho na masikio yao wanayaelekeza katika mechi yao ya Ligi Kuu kati yao na Mtibwa huko Morogoro.

Katika mechi ya Yanga na Zesco, vijana wa Jangwani wanajivunia uzoefu wa Kocha Mkuu George Lwandamina katika michuano ya kimataifa, rekodi yake ni kuifikisha Zesco hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana.

“Lwandamina amekuwa na sifa nzuri ya kutoa vipigo, hasa kwa timu za Waarabu, ambapo katika michuano iliyopita akiwa na Zesco, aliiwezesha kuvuka kundi ‘A’ lililokuwa na timu ngumu kama Al Ahly ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco na Asec Mimosas ya Ivory Coast,” amesema Mkwasa.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema klabu iko vizuri licha ya matatizo madogo madogo yaliyopo. Kuhusu tetesi kwamba klabu hiyo itasafiri kwa treni ya Tazara, amesema si kweli.

“Hizo ni propaganda za maadui wa Klabu ya Yanga lakini ni bora wasubiri taarifa rasmi kutoka katika mamlaka husika kama wanataka ukweli,” amesema Mwambusi.

Historia ya Yanga kimataifa

Licha ya kufanikiwa kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo na ile ya Kombe la Shirikisho, mara nyingi Yanga imekuwa ikishindwa kupiga hatua za mbali na kujikuta ikitolewa katika hatua za awali.

Kwa sasa klabu hiyo inashiriki michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara 25, huku wakiwa wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi mara moja na raundi nyinginezo wakiishia kwenye hatua za awali.

Mabingwa hao mara 26 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamekuwa wakizinyanyasa timu ndogo wanazopangiwa nazo hatua ya awali kutoka Comoro, Botswana au Zimbabwe, lakini safari yao hufikia ukingoni pale wanapokutana na miamba ya soka la Afrika.

Mwaka 2012, Yanga iliaga mapema Ligi ya Mabingwa, ambapo mchezo wa raundi ya kwanza walipangiwa na Klabu ya Zamalek ya Misri na kujikuta wakiambulia kipigo cha jumla ya mabao 2-1 katika mechi zote mbili.

Kabla ya fainali za mwaka jana, mara ya mwisho timu hiyo kushiriki Ligi ya Mabingwa ilikuwa ni mwaka 2014 ilipotolewa na National Al Ahly kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, baada ya kutoka sare ya mabao 1-1, Yanga wakishinda bao 1-0 nyumbani na katika mchezo wa marudiano Al Ahly nao wakashinda 1-0 na kuamuriwa ipigwe mikwaju ya matuta.

Awali Yanga iliitoa Komorizone ya Comoro kwa idadi kubwa ya mabao, mchezo huo ulimpa tuzo ya ufungaji bora aliyekuwa winga wa kikosi cha Wanajangwani hao, Mrisho Ngasa, ambaye alifunga ‘hart trick’ mbili kwenye mechi zote mbili.

By Jamhuri