Yanga yadhamiria kubeba makombe

Timu ya Yanga imedhamiria kuchukua makombe yote manne msimu huu baada ya kuichapa bao 1-0 Singida Big Stars na kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mchezo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa Liti Mjini Singida.

Yanga Sc wapo katika hatua ya fainali Kombe la Shirikisho barani Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) .

Yanga SC walianza mchezo kwa kubadilisha kikosi cha kwanza kwa kuwapumzisha nyota wake kujiandaa na Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baadhi ya wachezaji walioanza ni Mauya, Doumbia, Mzize na mlinda lango Metacha Mnata.

Kipindi cha pili Prof.Nabi alifanya mabadiliko ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza aliwaingiza Fiston Mayele, Kennedy Musonda , Tuisila Kisinda na Dikson Job mabadiliko hayo yalibadilisha mchezo na Yanga kuendelea kuishambulia Singida Big Stars.

Kuingia kwa wachezaji hao kuliipa Yanga SC faida na kupata bao dakika ya 82 likifungwa na mshambuliaji Fiston Mayele baada ya shuti la Dennis Nkane kupanguliwa na golikipa Benjamin Haule.

Kwa matokeo hayo Yanga Sc imetinga fainali na sasa itaenda kukutana na Azam FC ambao utachezwa uwanja wa Mkwakwani Tanga Juni mwaka huu.