Hadi naandika makala hii, mizogo ya tembo wanane imeonekana katika Kijiji cha Maaloni, Arash, Ngorongoro mkoani Arusha.

Miezi miwili, katika Kitongoji cha Karkamoru, Loliondo pekee twiga wanane wameuawa. Watuhumiwa wa ujangili wamekwisha kukamatwa, japo kuna taarifa kuwa wahusika wenyewe bado wamo mitaani.

Mauaji hayo ya twiga ni tofauti na haya ya tembo. Tembo wanakufa kwa namna inayotia shaka. Mizoga hii ina pembe. Huu ni ushahidi kuwa si majangili waliofanya uharamia huu, maana kama wangelikuwa wao, kitu muhimu kwao ni hizo pembe.

Nimeona ripoti ya uchunguzi wa kimaabara kutoka TVLA ya Desemba 4, mwaka huu kutoka Kituo cha Arusha. Majibu ya uchunguzi wa awali ni kwamba tembo hao hawakufa kwa ugonjwa wa kimeta. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba, ama kuna ugonjwa mpya unaowapata wanyama hao, au ni hujuma kutoka kwa wananchi, hasa wale wenye mashamba ndani ya Loliondo.

Naendelea kuyasema haya ya Loliondo kutokana na hatari ya kiuhifadhi inayoendelea katika Pori hili la Akiba ambalo sasa ni kama halina mwenyewe. Lawama kwa yote haya yanayotokea ni kwa serikali iliyopata kigugumizi cha kulifanya eneo hili liwe na ulinzi imara, hivyo kuleta tija ya uhifadhi kwa jamii ya Loliondo, Ngorongoro na taifa kwa jumla.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) haina kikosi kazi cha kulinda eneo hili. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) haina ruhusa kisheria ya kulilinda eneo hili. Kazi pekee ya ulinzi imeachwa ifanywe na wawekezaji ambao nao wanakatishwa tamaa kwa kigugumizi hiki cha serikali cha miaka miwili sasa cha kushindwa kutunga sheria ya kulilinda eneo hili.

Nampongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, kwa kutambua umuhimu wa Loliondo kwa uhai wa Serengeti. Dk. Kigwangalla wa leo si yule wa siku za mwanzo katika ofisi hii. Ameijua vizuri sana Loliondo, kiasi cha kuziafiki hoja za wahifadhi ambazo awali angedhani ‘wamenunuliwa’ na wawekezaji. Kwa msimamo wake wa uhifadhi, tayari ameshaanza kuundiwa zengwe na NGOs zenye hila. Anaonekana amenunuliwa, ilhali ukweli ni kwamba amejua ukweli mpana wa Loliondo. Bado naendelea kumhadharisha awe makini na Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mbunge wa Ngorongoro, maana hao kwa hoja wapo upande wa NGOs.

Kuna taarifa kuwa endapo eneo hili litatungiwa sheria maalumu na kuwekwa chini ya NCA, kwa kuanzia kila mwaka NCA itatoa Sh bilioni 4.8 kwa ajili ya maendeleo ya vijiji 14 vya Loliondo. Hizi ni fedha nyingi mno. NGOs hazitaki hiyo sheria! Unaweza kujiuliza, nini kinazisukuma kuzikataa fedha hizo? Jibu ni jepesi kabisa. Fedha hizi zitaingia serikalini na kufanya kazi za wananchi kwa manufaa ya wananchi. NGOs ziko radhi ziwe na WMA na fedha nyingi ziingie mifukoni mwao. Gambo na Nasha ndiyo wanayotaka hayo. Huo ndio ukweli.

Taarifa za karibuni zilisema rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ilikuwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Je, nini kinayakwamisha? Mkwamo huu unaifanya Loliondo iwe haina mwenyewe na matokeo yake ndiyo haya ya kuuawa tembo na twiga kila uchao. Hali ni mbaya.

Wakati kigugumizi hiki kikiendelea, NGOs zinahaha huku na kule kuibua vurugu mpya, kubwa na mbaya zaidi kwa Loliondo na Ngorongoro. Wiki kadhaa zilizopita Watanzania na Wakenya walizuru Uingereza kwenda ‘kusambaza sumu’ ya kupinga eneo hili kuhifadhiwa kisheria.

Waliokwenda ni Samwel Naingirya, Shomet ole Naigisa, Norang’rang Timan, Scholastica Kukutya (Mkenya) na wengine kadhaa. Diwani wa CCM Kata ya Ololosokwan yumo kwenye mpango huu. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro yumo pia kwenye mkakati huu. Hawa wana shirika jipya linaloitwa TEST walilolianzisha bila kujali mipaka ya nchi, kwa kazi moja ya kuendeleza mapambano Loliondo.

Hoja dhaifu inayotumiwa ni kuwa serikali imekusudia kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Ngorongoro ardhi yao. Huu ni uongo, lakini kimya cha serikali ndicho kinachohalalisha uongo huo uonekane ukweli mbele ya jumuiya ya kimataifa. Mengi ya kuichafua nchi yaliyozungumzwa huko ughaibuni na ujumbe huu nitayachapisha.

Migogoro inayoibuliwa ndani ya jamii Ngorongoro ni mtaji na chanzo cha kuombea fedha kwa wafadhili, na kamwe hali hii haitatulia hadi hapo serikali itakapoamua kwa dhati kuchukua uamuzi wenye manufaa kwa jamii na kwa nchi. Ngorongoro kama yalivyo maeneo mengine yenye hazina za kiuchumi, ni mali ya Watanzania wote, na kamwe si kwa ajili ya kundi moja tu.

Kuhakikiwa kwa NGOs si jambo linalotakiwa kabisa Ngorongoro. Wamiliki wake wanafanya vikao vingi kuweka mkakati wa kukabiliana na tamko la serikali. Kisingizio chao ni kuwa uhakiki unalenga kuwatetea wahifadhi na wawekezaji na kuwakandamiza wafugaji.

NGOs hizi zinapokea mabilioni ya shilingi na hakuna kazi yoyote ya maana inayofanywa ili kuwanufaisha wananchi maskini. NGOs zimebaki kuwa mlango wa mapato ya kuwanufaisha wenye nazo na familia zao.

Migogoro mingi imeendelea kuwapo kwa sababu NGOs hizi zina fedha zinazotumika kwa malengo tofauti na walivyoomba kutoka kwa wafadhili wao. Kama NGOs za sehemu nyingine nchini zimekubali kuhakikiwa, kwanini Ngorongoro wawe wababe?

Kimya cha serikali juu ya hatima ya Loliondo kinalifanya eneo hili lenye hazina kubwa kiuchumi liteketezwe. Mambo muhimu kwa nchi yanapaswa yaamuliwe kwa wakati. Kimya hiki kinaua ari ya wahifadhi na wawekezaji.

990 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!