WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea uharibifu wa makusudi ​wa miundombinu ya barabara na majengo unaofanywa na baadhi ya wananchi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja.
 
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu, Bw. Kiswaga Destery aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani dhidi ya wananchi wanaoharibu miundombinu ili wakauze kama vyuma chakavu kwa vile Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu hiyo.
 
Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia fedha nyingi sana kuboresha miundombinu mbalimbali nchini na kwamba kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda miundombinu hiyo.
 
“Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara na majengo ili kutolea huduma, Watanzania wote tunao wajibu wa kuilinda na endapo itatokea mtu anaihujumu miundombinu hii, Serikali hatuwezi kukaa kimya, lazima tutachukua hatua,” ameonya.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya papo kwa papo, Bungeni jijini Dodoma, Mei 17, 2018.
 
Amesema jukumu la ulinzi ni la Watanzania wote, na kila Mtanzania anayo dhamana ya ulinzi na usalama wa ndani ya nchi ikiwemo kuilinda miundombinu. “Juzi niliona kwenye televisheni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mheshimiwa Jaffo akishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga, wamekamata Fuso lililojazwa vyuma vilivyong’olewa kwenye barabara, ni vile ambavyo vinawekwa kwenye daraja na kingo za barabara,” amesema.
 
“Huu ni uharibifu ambao hatuwezi kuvumilia, na katika hili Watanzania lazima tuungane pamoja tukemee tabia hii. Tunatumia fedha nyingi kujenga kingo za barabara, kuashiria maeneo yenye hatari lakini Watanzania wengine wanakuja kung’oa kwa matumizi yao. Mimi naamini Mkoa wa Shinyanga utakuwa umechukua hatua kali dhidi yao,” amesema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo akizungumza na Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule, Bungeni jijini Dodoma, Mei 17, 2018.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Faustine Ndugulile, akijibu swali, Bungeni mjini Dodoma, Mei 17, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Madini, Angela Kairuki, Bungeni jijini Dodoma, Mei 17, 2018.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akijibu swali, Bungeni mjini Dodoma, Mei 17, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifurahi jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo, Bungeni jijini Dodoma, Mei 17, 2018.
Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, akizungumza Bungeni mjini Dodoma Mei 17, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Hanang, Mary Nagu, Bungeni jijini Dodoma, Mei 17, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia, Bungeni jijini Dodoma, Mei 17, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

By Jamhuri