Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Oktoba 8, 2026
UBORESHWAJI wa Daraja la Chalinze Mzee lililopo katika barabara ya Chalinze–Segera, mkoani Pwani, umefikia asilimia 90, huku Serikali mkoani humo ikiridhishwa na maboresho yanayoendelea kukabiliana na athari za mvua zinazotarajiwa kunyesha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Oktoba 8, 2026, ambalo lilikuwa likikabiliwa na changamoto ya maji ya mvua kubomoa kingo za mto na kuhatarisha usalama wa daraja.
Amesema maboresho hayo yatasaidia kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo, hususan katika kipindi cha mvua.
“Uboreshaji huu ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha maeneo yote korofi yanaimarishwa na kuwa tayari kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino,” amefafanua Nyongo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Pwani, Mhandisi Patrick Rambika, amesema hatua hiyo inalenga kuzuia maji kupanda juu ya barabara na wakati mwingine kuwalazimu madereva kusafiri kutoka upande mmoja kwenda mwingine, jambo linaloweza kuwa hatarishi.
Amesema TANROADS itaendelea kufuatilia maeneo yenye changamoto ili kuhakikisha yanapatiwa ufumbuzi na miundombinu ya barabara inaendelea kuwa salama kwa watumiaji.
Rambika amesema maeneo matatu korofi yaliyopo Chalinze yamefanyiwa maboresho kwa kiwango kikubwa, huku Daraja la Chalinze Mzee likifikia asilimia 90 ya utekelezaji.
Ameongeza kuwa TANROADS pia imeshughulikia eneo la Daraja la Ruvu Chini, kwa kusafisha mkondo wa maji na kuimarisha maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na mmomonyoko kwa kuweka mawe kuzuia maji yaliyokuwa yakisababisha kubomoka kwa kingo za mto.





