Iran imejibu pendekezo la usitishwaji mapigano na kufunguliwa Mlango Bahari wa Hormuz na kuelezea msimamo na matakwa yake na kusisitiza kuwa mazungumzo “hayaendani na masharti wala vitisho vya kutenda uhalifu wa kivita.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Esmaeil Baghaei amesema Tehran inazingatia matakwa yake kulingana na maslahi ya kitaifa ambayo tayari yamewasilishwa kupitia wapatanishi, na kuongeza kuwa matakwa ya awali ya Marekani kama vile mpango wenye vipengee 15 yamekataliwa kwa kuwa yalikuwa na “masharti kupita kiasi.”
“Kwa kuzingatia maslahi yetu, tumekuwa tukiweka wazi matakwa yetu kamili tuliyonayo na tunayoendelea kuwa nayo. Sikiliza, Iran haina hofu kuelezea waziwazi kile inachokiona kama madai yake halali na ya msingi. Serikali ya Jamhuri ya Iran inaweka wazi matakwa yake kwa ujasiri mkubwa, na kufanya hivyo hakupaswi kutafsiriwa kama ishara ya kusalimu amri mbele ya adui yetu.”
Baghaei amesema Iran imeandaa majibu yake na itatoa maelezo zaidi hapo baadae bila kutoa muda mahsusi.
Kwengineko shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia, IAEA, limethibitisha leo Jumatatu kuhusu athari za hivi karibuni za mashambulizi ya kijeshi karibu na kinu cha nyuklia cha Iran cha Bushehr, lakini likasema kiwanda chenyewe hakikuharibiwa.
IAEA imesema uthibitisho huo umetokana na uhakiki wake huru wa picha mpya za setilaiti na ufahamu wa kina wa eneo hilo, na kwamba shambulio moja lilipiga takriban mita 75 pekee kutoka kwenye eneo la kituo hicho.



