SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar leo Aprili 15, 2026, inatarajia kupokea ujumbe wa wataalamu wa sekta ya afya kutoka nchi mbalimbali kwa ziara maalum ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.

Ugeni huo unatarajiwa kuwasili na kushiriki ziara hiyo itakayofanyika kuanzia Aprili 15 hadi 17, 2026, ukilenga kuangalia mafanikio yaliyofikiwa na Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya, hususan kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Madinatul Al Bahr, Mbweni, Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema ziara hiyo ni sehemu ya ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza sekta ya afya.

Alisema wataalamu hao wanatoka katika nchi ya Madagascar, Ethiopia, Msumbiji na Zambia, na wanakusudia kujifunza mbinu bora za utoaji huduma za afya pamoja na kushuhudia hatua zilizopigwa katika mageuzi ya sekta hiyo Nchini.

“Ziara hii inalenga kuangalia mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya afya Zanzibar na kujifunza mbinu mbalimbali za utoaji huduma bora kwa wananchi,” amesema Dk. Saada.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kikamilifu kuwapokea wageni hao kwa kuwapatia fursa ya kujionea utekelezaji wa mifumo ya kisasa ya kidijitali katika sekta ya afya.

Miongoni mwa mifumo hiyo ni ile ya mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, pamoja na mifumo ya usimamizi wa rufaa na huduma za dharura, ambayo imechangia kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wakati.

Aidha, alifahamisha kuwa ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, huku ikitoa jukwaa la kubadilishana uzoefu, maarifa na ubunifu katika matumizi ya teknolojia za kisasa za afya.

Ziara hiyo ni ishara ya kutambua mafanikio yaliyopatikana Zanzibar katika kuimarisha mfumo wa afya kupitia uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika mifumo ya kidijitali, huduma za rufaa na dharura, pamoja na maendeleo ya rasilimali watu.