WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kugharamia maadhimisho ya Sherehe za Muungano mwaka huu, zitumike kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Ameyasema hayo, leo Jumatatu, Aprili 20, 2026 Ofisini kwake Mlimwa Jijini Dodoma alipokuwa akiuarifu umma kuhusu maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakavyofanyika.
“Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Muungano yatafanyika katika ngazi ya Mikoa yote nchini ambapo Viongozi Wakuu wa Kitaifa watafanya shughuli za kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo” Amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu amesema imeelekezwa kuwa Wakuu wa Mikoa watembelee, waweke Mawe ya Msingi na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kushiriki shughuli za usafi wa mazingira, kupanda miti na kufanya mashindano ya michezo mbalimbali.
“Ninamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuelekeza fedha ambazo zingetumika kwa kufanya Maadhimisho haya kwa gwaride na michezo ya halaiki zitumike katika shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.” Ameongeza Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu.
Pia Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ameagiza majengo yote ya Serikali kunakshiwa kwa rangi za bendera ya Taifa kuanzia tarehe 20 Aprili, 2026 hadi tarehe 26 Aprili, 2026 siku ya kilele. “Majengo yote ya Serikali Tanzania Bara yapambwe kwa vitambaa vya rangi ya bendera ya Taifa, picha za Waasisi wa Muungano na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Amesema Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar, majengo yapambwe kwa vitambaa vya rangi sahihi za Bendera ya Taifa, Picha za Waasisi wa Muungano na Picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Picha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
“Nitumie fursa hii kuwahamasisha wananchi wote kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za kijamii, midahalo na makongamano katika kila mkoa ili kujadili maendeleo endelevu yaliyofikiwa na nchi yetu katika kipindi cha miaka 62 ya muungano. Aidha, ni muhimu Wananchi wote waendelee kuulinda uungano wetu ili kudumisha umoja, amani na mshikamano wetu.” Amehimiza Waziri Mkuu.
Shughuli nyingine zitakazoambatana na Maadhimisho haya ni Pamoja na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali; mashindano ya uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari; mahojiano maalum na wazee maarufu; midahalo na makongamano kuhusu muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi sasa.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni: “MIAKA 62 YA MUUNGANO: AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO NI MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU.”


