Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Kigoda–Ngwale katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, utakaowanufaisha wananchi 821 wa kijiji cha Kigoda na sehemu ya kijiji cha Ndwati, ambao awali walikuwa wakipata maji yasiyo salama kutoka mabwawa yaliyopo umbali wa takribani kilometa 2.5.
Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umefikia asilimia 90 ya utekelezaji, ukiwa na thamani ya shilingi milioni 546.7, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi milioni 254.4 zimelipwa kwa mkandarasi, Lukedan Co. Ltd.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Mwang’onda aliitaka RUWASA kuhakikisha inakamilisha mradi huo kwa wakati na kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi .
Aidha, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga na kupeleka fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan sekta ya maji.
“Miradi hii ni mikubwa na inagharimu fedha nyingi, hivyo niwaombe wananchi wawe walinzi wa kuitunza ili iweze kudumu na kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Mwang’onda.
Katika hatua nyingine, Mwenge wa Uhuru umeweka mawe ya msingi katika miradi mingine ikiwemo ujenzi wa jengo la huduma ya mionzi, vyumba vinne vya madarasa na ofisi mbili katika Shule ya Sekondari Disunyara, pamoja na kiwanda cha nondo na vifaa vya ujenzi cha Gaini Co. Ltd chenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 120.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, akipokea Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya Shule ya Msingi Gumba, Kata ya Gwata, alisema jumla ya miradi 26 yenye thamani ya shilingi bilioni 162 inatarajiwa kupitiwa katika Manispaa ya Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Alifafanua kuwa kati ya miradi hiyo, miradi 13 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 121.392 ipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.









