
NDEJEMBI AIPONGEZA REA
📌Atoa wito kwa Wabunge kutembelea Banda la Maonesho
📌Mkurugenzi Mkuu REA aahidi kutekeleza miradi kwa wakati
📍Bungeni – Jijini Dodoma
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake hususan wa maeneo ya vijijini kupitia Usambazaji wa Nishati ya Umeme pamoja na Nishati Safi ya Kupikia.
Ametoa pongezi hizo Aprili 20, 2026 Jijini Dodoma alipotembelea Banda la REA katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea ndani ya viwanja vya Bunge Jijini Dodoma
“Hongereni sana wataalam mnatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwafikishia wananchi wake kote nchini Nishati,” amepongeza Mhe. Ndejembi
Aidha, Mhe. Ndejembi amewaalika Waheshimiwa Wabunge kutembelea Banda la Maonesho la Nishati ili kushuhudia kazi kubwa inayotekelezwa na Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake.
“Tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kutembelea Maonesho haya pamoja na wageni wao kwani ni fursa nzuri ya kukutana na wataalam na Kujadili hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi katika Majimbo yao,” amesema Mhe. Ndejembi.
Amesema Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinashiriki na kwamba wataalam wapo tayari na ni fursa kwa Wabunge kukutana na wataalam hao ili kujadili changamoto zilizopo na kutazama namna bora ya kuzipatia ufumbuzi.
“Lengo la Maonesho haya ni kuonyesha kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuna mengi ya kujifunza kwenye banda hili,” amesema Mhe. Ndejembi
Halikadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy amemhakikishia Waziri Ndejembi kuwa, miradi yote inayotekelezwa kwa sasa itakamilika kwa wakati na REA imejipanga kikamilifu kutekeleza miradi hiyo.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni miongoni mwa Taasisi zinazoshiriki katika Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 20 Aprili, 2026.







