Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda, ameweka jiwe la msingi katika kiwanda cha Doweicare Technology Ltd kilichopo Kata ya Misugusugu, Manispaa ya Kibaha, huku akiipongeza Serikali kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji
Kiwanda hicho kinajishughulisha na utengenezaji na usambazaji wa bidhaa za softcare kwa matumizi ya usafi, ikiwemo nepi za watoto na taulo za kike, kikiwa kimewekeza dola za Marekani milioni 16, sawa na takribani shilingi bilioni 40.
Akikagua na kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho Aprili 21, 2026, Mwang’onda aligawa taulo za kike 6,000 kwa wanafunzi 1,000, zitakazowatosheleza kwa muda wa miezi sita.
Aidha, aliipongeza Manispaa ya Kibaha pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuendelea kumpa ushirikiano Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia na kuimarisha sekta za uwekezaji na viwanda.
Awali, akipokea Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya Shule ya Msingi Visiga, Kata ya Visiga, Manispaa ya Kibaha, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema miradi nane yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 41.1 imezinduliwa, kukaguliwa na kuwekwa mawe ya msingi.
Miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya Kongowe–Forest, ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Picha ya Ndege, na huduma za afya katika Zahanati ya Kilimahewa yenye thamani ya shilingi milioni 284.6.
Miradi mingine ni kisima kirefu cha maji safi katika Shule ya Msingi Tangini, mradi wa Kibaha Shopping Mall pamoja na mradi wa CJ-Chalya Plumbing Services unaohusisha shughuli za kikundi katika utengenezaji na uuzaji wa mabomba ya maji.
Mwenge wa Uhuru upo katika siku ya nne tangu kupokelewa mkoani Pwani Aprili 18, 2026, na unatarajiwa kupokelewa wilayani Mafia Aprili 22, 2026.









