Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema kuwa tume hiyo imebaini kuwepo kwa tofauti kati ya chanzo na kichocheo cha ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu, ambapo chanzo ni sababu za muda mrefu zinazojenga matatizo katika jamii huku kichocheo kikiwa ni msukumo wa moja kwa moja wa matukio hayo.
Akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jaji Chande, amesema kuwa tume ilipokea na kuchakata jumla ya maeneo 31 yaliyotajwa na mashahidi kuwa ni vyanzo vya ghasia hizo, na baada ya uchambuzi imebaini vyanzo vitano na vichocheo nane vilivyochangia matukio ya Oktoba 29.
Aidha amebainisha kuwa miongoni mwa vyanzo hivyo ni masuala ya kisiasa yanayohusisha madai ya katiba mpya, demokrasia ya vyama vingi, malalamiko ndani ya vyama vya siasa pamoja na madai ya maboresho ya tume huru ya uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi.
Pia amesema kuwa vipo vyanzo vya kijamii vinavyohusisha changamoto za kiuchumi kama ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, mazingira yasiyo rafiki ya biashara na uwekezaji pamoja na utitiri wa tozo na kodi.
Ameongeza kuwa tume imebaini pia changamoto za kijamii zinazohusisha mmomonyoko wa maadili, kushuka kwa uzalendo, pamoja na malalamiko ya wananchi kuhusu rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na madai ya utekaji na kupotea kwa watu.
Aidha amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, kati ya mwaka 2003 hadi 2005, watu 758 walipotea, kutekwa au kujiteka, ambapo 113 walipatikana na mashauri nane kufunguliwa huku 445 hawajapatikana, hali inayotoa taswira ya ukubwa wa changamoto hiyo katika jamii.
Pia amesema kuwa miongoni mwa vyanzo vingine ni utendaji usioridhisha wa baadhi ya watumishi wa umma hususan ngazi za chini pamoja na kushindwa kutatua kero za wananchi kwa wakati na utekelezaji hafifu wa mapendekezo ya tume zilizopita.
Ameongeza kuwa tume pia imebaini masuala ya uhusiano wa kimataifa ambapo mataifa hutanguliza maslahi yao na kutumia mikakati mbalimbali katika kuimarisha nafasi zao kiuchumi na kisiasa katika nchi zinazoendelea.
Aidha amebainisha kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi kama fursa ya kuwahamasisha kushiriki ghasia kupitia kaulimbiu na matamko mbalimbali.
Pia amesema kuwa vichocheo vya ghasia hizo vimegawanyika katika makundi matatu, ambapo kundi la kwanza linahusisha matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ikiwemo kuhamasisha kutoshiriki uchaguzi na kupanga mbinu za kuzuia mchakato wa uchaguzi.
Ameongeza kuwa baadhi ya washiriki walitumia mitandao hiyo kurusha picha na video za matukio ya vurugu ili kuchochea hisia za wananchi na kuongeza ushiriki wa ghasia.
Aidha amebainisha kuwa kundi la pili la vichocheo linahusisha kaulimbiu zilizotumiwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati zenye lengo la kushinikiza mabadiliko ya kisiasa, ikiwemo kauli mbalimbali zilizohamasisha kutofanyika kwa uchaguzi bila mabadiliko.
Akiongeza kuwa kundi la tatu linahusisha baadhi ya watu waliokuwa na malengo ya kisiasa baada ya majina yao kukatwa katika mchakato wa ndani ya vyama, ambapo walihusishwa na kuhamasisha au kushiriki ghasia kwa lengo la kushinikiza mabadiliko ya mifumo ya uteuzi wa wagombea.



